Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga,akizungumza Novemba 22, 2023 wakati akifungua kikao cha kupokea miradi sita iliyotekelezwa katika Wilaya tatu mkoani Singida na Shirika lisilo la kiserikali la Sustainable Environment Management Action (SEMA) kwa kushirikiana na Shirika la Stromme Foundation . Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Sema, Ivo Manyaku na Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Singida, Romwald Mwendi.
......................................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Sustainable Environment Management Action (SEMA) limekabidhi kwa Serikali ya Mkoa wa Singida miradi sita ambayo ilikuwa ikiitekeleza kwenye Halmashauri tatu za Wilaya ya Iramba, Ikungi na Manyoni ili ziiendeleze kuisimamia baada ya shirika hilo kumaliza miaka mitano ya utekelezaji ambao utafikia tamati Desemba 31, 2023.
Miradi hiyo ambayo ni ya kimtambuka ilikuwa ikitekelezwa na
shirika hilo kuanzia mwaka 2019- 2023 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali likiwemo Shirika
la Stromme Foundation ambayo iligharimu zaidi ya Sh.Bilioni 4.5
kuitekeleza.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ivo Manyaku akizungumza
Novemba 22, 2023 katika kikao cha kukabidhi miradi hiyo kwa Serikali, aliitaja
miradi iliyotekelezwa katika kipindi hicho ni pamoja na uwezeshaji jamii kiuchumi, mradi wa kuweka akiba na kukopa (WEKEZA), mradi
wa Bonga (NJOO TUONGEE), mradi wa elimu ya mafunzo ya ufundi kwa vijana
(TUNAWEZA), mradi wa elimu ya awali na makuzi, mradi wa Kuzijengea uwezo asasi
za kiraia na mradi wa uwezeshaji jamii Kilimo biashara.
Alisema miradi hiyo imewanufaisha watu takribani 450,000 ambayo ililenga kukabiliana na wimbi kubwa la umasikini kwenye makundi ya jamii, likiwemo kundi la vijana, wasichana na watu wenye mahitaji maalumu.
Manyaku alitaja malengo mengine ya miradi hiyo ilikuwa ni kuboresha uchumi
kwa walengwa, afya na lishe, elimu jumuishi, huduma ya maji na usafi wa
mazingira, utawala bora, kilimo na mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma
Mganga ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Rasilimali Watu, Stephen, Pancras aliwataka maafisa maendeleo ya
jamii wa halmashauri za wilaya mkoani hapa kuhakikisha wanawahamasisha wananchi
kujiunga kwenye vikundi ili idadi ya wanufaika wa miradi hiyo iwe kubwa kwa
kuzingatia kuwa kupitia vikundi hivyo ndimo yanamopatikana maendeleo.
Pancras alipongeza juhudi kubwa za wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani
hapa likiwamo shirika la Sema na Stromme Foundation ambayo kwa
kiwango kikubwa yameleta tija na ustawi wa maisha kwa wana-Singida.
“Serikali itaendelea kushirikiana na mashirika haya na mengine na wadau wa
maendeleo mtakao jitokeza lengo ni kuhakikisha mnaisaidia jamii,” alisema
Pancras.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Singida Dkt. Elpidius Baganda alilipongeza shirika hilo kwa kutekeleza miradi ya sekta ya elimu na kuwa elimu ikitolewa sawa sawa ndio suluhisho la mambo mengi katika maisha ya wanadamu.
Aidha Baganda alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali chini ya Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yanayafanya mashirika
hayo yasiyokuwa ya kiserikali kutekeleza miradi yao pasipo bughudha zozote.
Baadhi ya viongozi na maafisa maendeleo ya jamii wanaosimamia na kukagua miradi
hiyo waliohudhuria kikao hicho walilipongeza Shirika la Sema kwa kuwa kinara mkoani
hapa katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa viwango vya juu na thamani
halisi inayolingana na fedha zilizotolewa na wafadhili.
Shirika la Sema ni Shirika lisilokuwa la Kiserikali lililosajiliwa Machi 10,1998 na kuanza rasmi shughuli za utekelezaji Januari 1,2000 na lilipata hati ya ukubalifu (Certificate of Compliance) Machi 9, 2006 na makao yake makuu yapo Manispaa ya Singida eneo la Utemini (Mtaa wa Viwanda).
Post A Comment: