Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Sustainable Environment Management
Action (SEMA) lenye makao yake makuu mkoani Singida kwa kushirikiana
na Shirika la Stromme
Foundation Tanzania kupitia mradi wa Kilimo Biashara wa ELCAP katika kipindi cha miaka
miwili ya utekelezaji wa mradi huo wamepata mafanikio makubwa ya uongezaji
uzalishaji wa mazao kwa kutoa elimu za teknolojia mbalimbali za kilimo.
Mkurugenzi wa SEMA, Ivo
Manyaku akizungumza Novemba 7, 2023 kwenye kikao kazi cha kutathimini utekelezaji
wa mradi huo wa miaka mitano ulioanza
Septemba 20, 2021 ambao unatarajia kumalizika Mwezi Juni, 2026 umekuwa na
mafanikio makubwa kwa wakulima.
Alisema lengo la mradi huo
ni kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha kwa ubora zaidi na kupata mazao mengi
katika eneo dogo.
Manyaku alisema mradi huo ni mahususi kwa vijana na wanawake na ni
muendelezo wa vikundi vilivyokuwa vikitumika katika mradi wa awali wa kuweka na
kukopa na sasa wanawatoa katika eneo hilo na kuwaingiza kwenye uzalishaji wenye tija na
kuongeza thamani kupitia mazao ya kilimo ambayo ni mahindi, alizeti, mtama na
mbaazi.
Aidha, Manyaku alisema kupitia mradi huo wamefanikiwa kuwatafutia wakulima
masoko kwa kuwaunganisha na wadau mbalimbali na wafanyabiashara .
Akitaja mafanikio mengine kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo wakulima
walikuwa wakipata magunia ya mahindi kati ya sita hadi saba kwa heka moja
lakini sasa wanapata magunia 15 hadi 20 na akamtaja mmoja wa wakulima hao
kutoka Wilaya ya Ikungi kuwa alipata magunia 10 katika nusu heka.
Alisema lengo la mradi huo ni kuwafikia wakulima 6000 na kati ya hao
asilimia 40 wawe vijana na asilimia mbili watu wenye ulemavu na kuwa umejikita
kuhakikisha kuwa teknolojia wanazo wapa zinaendelea kuwasaidia wakulima hata
baada ya mradi huo kumalizika.
Alisema pamoja na kuwa na lengo la kuwafikia wakulima 6000 lakini kwa
kupitia mnyororo wa thamani wanatamani kuwafikia wakulima 10,000 katika wilaya
ambazo unafanyika mradi huo ambazo ni Iramba, Ikungi na Manyoni na kuwa gharama
ya mradi huo ni Sh.Bilioni 4.5.
Alisema mradi huo unatekelezwa na SEMA kwa kushirikiana na Stromme Foundation na nchi ya Norway pamoja na
washirika wao wa kimkakati, NGI, CSFS na NMBU ambao wanawawezesha kuwapa teknolojia.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga ambaye alikuwa mgeni rasmi alishiriki kikao hicho na alitoa maoni yake namna ya kuboresha zaidi mradi huo ambapo alipongeza mashirika hayo kwa kuusaidia Mkoa wa
Singida katika sekta ya kilimo.
“Katika mradi huu ni Singida peke yake ndiyo inasaidiwa kuhakikisha
inaboresha kilimo ili kuongeza uzalishaji na hasa kwa kutumia teknolojia
inayokwenda kuhifadhi maji katika mashamba yetu na kurutubisha ardhi na
kuboresha maisha ya familia zetu,” alisema Mganga.
Alisema kwa kuwa mradi huo una walenga wakulima wadogo hasa wanawake
na vijana katika wilaya za Ikungi, Iramba na Manyoni anaamini kutokana na kuwa
wepesi wa kuelewa watakwenda kuleta mabadiliko chanya kwenye familia zao kwani
wakiwezeshwa kupata mikopo na mbegu bora mashamba yao yanakwenda kuwa dhahabu
katika Mkoa wa Singida.
Pamoja na mambo mengine alishauri mradi huo uweze kufika mpaka shule za msingi na sekondari.kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti Wizara ya Kilimo,
Mohammed Chikawe aliyashukuru mashirika hayo kwa kuungamkono jitihada za
Serikali katika sekta ya kilimo mkoani hapa na kueleza mradi huo unatekelezwa
vizuri ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau hao wa maendeleo kuusambaza
na kwenye mikoa mingine ili nayo iweze kupata teknolojia hiyo ya uzalishaji wa
mazao na kuongeza thamani pamoja na kuwatafutia masoko kama ilivyofanya katika
Mkoa wa Singida.
Wajasiriamali na wanufaika wa mradi huo Anna Ntandu kutoka Wilaya ya Ikungi
na Rehema Mwaliwa kutoka Kata ya Iseke wilayani Ikungi waliyashukuru mashirika
hayo kwa kuwapa mafunzo ya kilimo biashara ambayo yamewakomboa kiuchumi na
kuweza kujikimu kimaisha na kusomesha watoto wao.
“Changamoto kubwa tuliyonayo ni vifaa vya kufanyia kazi, mtaji na masoko ya uhakika kwa mfano mimi nalazimika kutumia sufuria kwa ajili ya kuoka mkate badala ya oveni naomba tunapo hitimu mafunzo tuwe tunawezeshwa vifaa hivyo hata kwa kukopeshwa,” alisema Mwaliwa.
Post A Comment: