Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini na Mbunge wa Jimbo la Butiama leo Novemba 14, 2023 ameshiriki Ibada ya mazishi ya Marehemu Edward Magige ambaye ni Mjukuu wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, iliyofanyika Kijijini kwao Wilayani Butiama Mkoani Mara.
Akizungumza katika mazishi hayo, Naibu Waziri Sagini ametoa pole kwa familia, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wafanyakazi wa NIDA Mkoa wa Shinyanga, ndugu, jamaa na marafiki na kuwaomba wazidi kumuombea aendelee kupumzika kwa amani.
"Baada ya kupata taarifa ya ajali pia nikaarifiwa kuwa alikuwa ni mtumishi wa NIDA huko Mkoani Shinyanga mimi kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi pia natoa pole kwa Mkurugenzi Mkuu na Watumishi wote," Amesema Sagini.
Ikumbukwe kuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ni moja kati ya chombo kilichopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo Marehemu alikuwa akikitumikia mpaka umauti ulipomfika mnamo Novemba 11, 2023 kwa ajali iliyotokea huko Mkoani Shinyanga, ambapo unakuwa ni msiba wa pili kwa mwezi mmoja tangu kutokea kwa msiba wa kwanza wa Marehemu Daudi Charles Mkongoro ambaye ni Mjukuu wa Baba wa Taifa na mtoto wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere aliyefariki Oktoba 29, 2023 kwa ajali ya gari iliyotokea katika barabara ya bypass Jijini Arusha.
Aidha Viongozi mbalimbali wa Kiserikali, Kidini na Kisiasa walishiriki mazishi hayo akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Butiama Moses Kaegele, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoani Mara Julius Masubo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ambaye pia ni baba mdogo wa marehemu Peter Wanzagi na Chifu wa Kabila la Wazanaki Japhet Wanzagi.
Post A Comment: