Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewaagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza kasi ya kuwaunganishia umeme wananchi vijijini katika maeneo ambayo tayari yamefikiwa na miradi ya usambazaji umeme ili miradi hiyo iweze kuwa na tija.
Amesema hayo tarehe 7 Novemba, 2023 Jijini Dodoma wakati wa kikao chake na Uongozi wa REA kilicholenga kupata taarifa za utekelezaji wa Miradi ya Nishati Vijijini na mipango iliyopo katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Haipendezi kuona mradi umefika katika kijiji na umekamilika lakini unakuta kaya tano au kumi tu zimeunganishwa, hii hailingani na nguvu iliyotumika kuufikisha mradi huo katika Kijiji husika, hivyo angalieni upya namna bora ya kuwahamasisha wananchi ili wajiunge na huduma hii,” amesisitiza Kapinga.
Amewasisitiza kuwa, suala la kuunganisha wateja walichukue kwa uzito mkubwa kama wanavyosimamia upelekaji wa umeme katika Vijiji na hii italeta matokeo chanya ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Tumieni njia mbalimbali katika kuwafikia wananchi ikiwemo kuungana nao katika mikusanyiko ya tamaduni zao za asili kama vile kwenye ngoma na sehemu nyingine kama hizo kulingana na maeneo husika na waelezeni ukweli kuwa gharama za kuunganisha umeme vijijini ni shilingi 27,000 ili waone njia bora ya kupata hizo fedha ili waweze kuunganishiwa umeme”, amesema Kapinga.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri ameielekeza REA kuwajengea uwezo Wasimamizi wa Miradi ya Umeme Vijijini ili waifahamu ipasavyo miradi hiyo na hivyo waongeze ufanisi katika kuwasimamia vyema Wakandarasi wanaotekeleza miradi husika.
Amesema kuwa, wasimamizi hao wanatakiwa kufahamu maeneo ya miradi yao na waanze kazi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi kuanzia pale ambapo Serikali inatoa fedha na kama kuna changamoto ama vikwazo vyovyote waweze kuvishughulikia mapema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amemueleza Naibu Waziri huyo kuhusu utekelezaji wa Miradi ya Nishati Vijijini iliyotekelezwa na inayotarajiwa kutekelezwa ambapo amemueleza Mhe. Kapinga kuwa, REA imepokea maelekezo aliyotoa kwa utekelezaji ili kuzidi kuboresha Sekta ya Nishati vijijini.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka na Viongozi wengine Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na REA.
Post A Comment: