Waziri wa Elimu, Sayansi na teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema serikali inatambua umuhimu wa Mabaraza ya Wahitimu na Jumuiya mbalimbali katika Vyuo Vikuu, katika kuchangia Maendeleo ya miradi mbalimbali katika Vyuo husika.
Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo leo Novemba 22, 2023 mjini Morogoro wakati akihutubia Baraza la Wahitimu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe ambapo amesema serikali inajivunia michango ya Wajumbe wa Baraza hilo, ikiwemo mchango wa ujenzi wa mabweni kwa ajili ya Wanafunzi.
Prof. amesema lakini pia "nawapongeza kufikia katika hatua za mwisho za kuanzisha mfuko wa ufadhili kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wasio na uwezo kugharamia masomo, na kwamba Sera ya mfuko huo tayari imeandaliwa na kupitishwa na ngazi husika nawapongeza sana" alisema Prof. Mkenda.
Wakati huo Prof. Mkenda amekipongeza Chuo hicho kwa kuanzisha Taasisi ya Mafunzo ya serikali, na kwamba hatua hiyo itaimarisha utolewaji wa huduma bora katika ngazi mbalimbali.
"Ni muhimu Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia wazo hili la kuanzisha taasisi ya Mafunzo Serikalini, iendelee na utamaduni wa kutoa huduma ya kuwajengea uwezo viongozi wetu, hasa kwenye ngazi za kati na chini" alisema Prof. Mkenda
Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Prof. Peter Msofe ameeleza kuwa Wizara inaona umuhimu mkubwa kutika kudumisha mahusiano ya karibu na Vyuo Vikuu katika kusimamia dhana ya elimu ya juu nchini.
"Tunatambua kuwa Vyuo Vikuu ni nguzo muhimu katika Maendeleo ya taifa letu, na ndio maana tunajitahidi sana kuhakikisha tunaweka mazingira bora ya kujifunza na kujifunzia" alieleza Prof. Msofe.
Amesema Elimu ya juu inapaswa kupewa kipaumbele katika kuhakikisha ubora wa Elimu unazingatiwa kwa kina na kwa wakati wote.
Nae Rais wa Baraza la Wahitimu katika Chuo Kikuu Mzumbe CPA. Rudovick Utoah ameipongeza serikali kwa kuendelea kusimamia mageuzi makubwa yenye mchango chanya katika sekta ya Elimu kwa kuzingatia viwango vya juu.
"Kazi inayofanya Wizara ya elimu, ambayo sisi ni wadau tunaithamini sana kwa namna inavyoshughulikia Taifa hili katika sekta ya Elimu, Sayansi na teknolojia Kwa niaba ya Mhe. Rais.
Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za kitaaluma Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof. William Mwegoha amesema Chuo hicho kinaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuhuisha mitaala iweze kuakisi mabadiliko makubwa yanayotarajiwa katika taifa hilo.
"Tunatambua mageuzi haya yanaakisi malengo ya serikali ya awamu ya Sita ambayo inasisita umuhimu wa Elimu inayotolewa katika ngazi zote nchini, kukidhi mahitaji ya jamii katika taifa letu" amebainisha Prof. Mwegoha.
Post A Comment: