Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amewapongeza Wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Masomo 2023/24 waliochaguliwa kujiunga na Chuo huku akieleza kuwa Chuo kinachotoa mafunzo bora katika fani mbalimbali za kitaaluma pamoja na mafunzo maalumu ya Uongozi, Maadili, Utawala bora, Uzalendo na Utaifa.
Akizungumza hii leo Katika kikao cha kuwakaribisha Wanafunzi wa Mwaka wa kwanza wa masomo 2023/24 katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada amewataka Wanafunzi kusoma kwa Juhudi na Maarifa na kuzingatia maelekezo yote wanayopewa na Waalimu pamoja na viongozi wa Chuo.
Prof. Mwakalila amewataka Wanafunzi kuhakikisha wanakuwa waadilifu, Waaminifu na Wazalendo kwa Chuo na Taifa kwa ujumla, kulipa ada kwa wakati na kujiepusha na tabia ya kugushi na kuazimana vitambulisho, kujiepusha na tabia ya udanganyifu katika mitihani, na kuhakikisha wanazingatia mambo ya msingi yaliyowaleta chuoni ya kupata maarifa bora yatakayowasaidia katika maisha.
Amewataka Wanafunzi Kujiepusha na makundi ya Uchochezi, Migogoro isiyo ya lazima na makundi ambayo hayana tija kwao na chuo kwa ujumla, kuheshimu Wafanyakazi, Waalimu na Wanafunzi wenzao.
Prof. Mwakalila ametoa wito kwa Wahadhiri i na Wafanyakazi wote wa Chuo kuendelea kutoa huduma bora kwa wanafunzi wote kwa kuzingatia Uadilifu, Uaminifu na Uzalendo kwa maslahi ya Chuo na Taifa kwa ujumla.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE
Post A Comment: