Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani) wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa umeme wa
.................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiongozwa na Makamu
Mwenyekiti Japhet Hasunga imeridhishwa na hatua iliyochuliwa na Seriakali ya kutumia fedha zake
za ndani kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na
kusafirisha umeme mkubwa cha Shinyanga kupitia mradi wa Backbone Transmission
Investment Project (BTIP), unaosimamiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
Hasunga alitoa pongezi hizo wakati kamati
hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo mkoani Singida Novemba 12, 2023 ambao ulisimama utekelezaji wake
kutokana na changamoto kadhaa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Hasunga alisema kamati hiyo imefanya ziara hiyo ili kujiridhisha na utekelezaji wa mradi huo ambao unahusisha kuviongezea uwezo
vituo vya kupokea na kupoza umeme mkubwa katika mikoa ya Iringa, Singida,
Dodoma na Shinyanga kutoka umeme mkubwa wa Kilovoti 220 kwenda umeme mkubwa wa
kilovoti 400.
Alisema lengo la mradi huo ni kuunganisha
nchi ya Tanzania na nchi ya Kenya ambao utaenda hadi Ethiopia na pia
kuunganisha nchi ya Tanzania na Zambia yaani nchi za Kusini mwa Afrika.
"Mwaka jana tulikuja hapa lakini
tulipata maelezo kiundani tuliona kulikuwa na changamoto katika utekelezaji wa
huu mradi na changamoto kubwa zilikuwa mbili ya kwanza ni kujitoa kwa baadhi ya
wafadhili ambao walikuwa wameahidi kutoa fedha hivyo kuathiri mradi huo na
kushindwa kukamilika," alisema Hasunga.
Hasunga aliongeza kuwa wakati wafadhili
hao wakijitoa tayari Serikali ilikuwa imekwisha tumia dola za Kimarekani zaidi
ya Milioni 400 kujenga miundombinu mbalimbali hadi nchini Kenya.
Alisema hiyo ilikuwa ni changamoto ya
kwanza lakini changamoto ya pili ilikuwa kituo cha kupozea umeme cha Shinyanga
kisingeweza kujengwa baada ya wafadhili hao kujitoa pamoja na kituo cha Iringa
ambacho kingeunganisha hadi Tunduma mkoani Mbeya.
Hasunga alisema kutokana na jambo hilo
kamati hiyo iliona zile fedha zilizotolewa mara ya kwanza na kujenga
miundombinu hiyo ya Shinyanga, Iringa na ile ya Tunduma kama isingekamilika
zingeonekana hazina thamani kwa sababu ya kutofiKIwa kwa malengo yaliyokusudiwa.
" Leo tumekuja kujiridhisha kuona maendeleo ya utekelezaji wa mradi huu na wote tumeshuhudia
na kuelezwa kuwa Serikali imeamua kujenga kituo cha Shinyanga kwa fedha za
ndani ili kuhakikisha mikoa ya Kanda ya Ziwa inaunganishwa katika suala hili la
nishati iliyotimilifu jambo ambalo tumelifurahia," alisema Hasunga.
Alisema jambo la pili ni mradi wa TAZA
kutoka Iringa hadi Zambia nao upo katika hatua za manunuzi ya kumpata
mkandarasi ambapo ukikamilika utaunganisha mikoa ya Kusini Magharibi ambayo ni
Songwe, Rukwa, Katavi , Kigoma na kuunganisha Nyakanazi hatua ambazo kamati
hiyo ilitaka ipate maelezo ya kina namna gani Serikali imejipanga kutekeleza
jambo hilo na wao wameziona jitihada zilizochuliwa hivyo wanaipongeza.
Hasunga alisema watafuatilia kwa karibu
kuona mradi huo una kamilika kwa muda uliopangwa ili watanzania waweze kuona
manufaa ya miradi hiyo.
Kamati hiyo imetoa ushauri kwa Serikali
kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kwani imejifunza miradi mingi inachukua muda
mrefu tofauti na ile iliyokubalika mara ya kwanza na hivyo kusababisha ongezeko
la gharama kubwa.
Akitoa taarifa mbele ya kamati hiyo
Mratibu wa mradi huo wa BTIP, Mhandisi Peter Kigadye alisema mradi huo
ulianzishwa mwaka 2014 baada ya marais wa Kenya, Tanzania na Zambia kukaa pamoja
na kuzungumza masuala mbalimbali na mahusiano ya nishati hiyo na namna ya kuuziana umeme
kutokana na kila nchi kuwa na gharama na vyanzo tofauti katika nchi za Afrika
Mashariki.
Mhandisi Kigadye alisema katika kikao
hicho Kenya na Zambia wakawa wameungana katika jambo hilo na kila nchi
ilitakiwa ijenge miundombinu kwa gharama zake ambapo wakenya walitengeneza
miundombinu na kuiunganisha na Ethiopia na Tanzania kuunganisha na nchi zote za
Kaskazini.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Shirika hilo, Mhandisi Dkt. Cosmas Masawe akizungumza kwa niaba ya
mwenyekiti huyo , aliishukuru kamati hiyo kwa kutembelea na kuona utekelezaji
wa mradi huo.
Aidha, aliomba kamati hiyo wanapotekeleza
miradi mbalimbali Taasisi nyingine za Serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ziwe zinawaondolea kodi na ushuru
mbalimbali wakati wa kusafirisha vifaa vyao na kuwa mara nyingi mchakato wake umekuwa ukichukua
muda mwingi na kujikuta wakitekeleza kazi zao nje ya muda na kwa hasara wakati
kazi inayofanywa ni ya serikali.
Mhandisi Masawe alitolea mfano nchi ya
Kenya taasisi nyingine ya Serikali inapotekeleza mradi umetengenezwa utaratibu
wakutozitoza ushuru kwa kuzingatia kuwa mradi husika upo chini ya Serikali.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Japhet Hasunga alipokea ombi hilo na kuahidi kulifanyia kazi kwa kushirikisha wahusika na taasisi zingine ilikuona namna bora ya kulizungumzia kwani miradi hiyo inayotekelezwa ni ya Serikali kwa ajili ya wananchi hivyo kuna kila sababu ya kuviondoa vikwazo hivyo kwa maslahi ya nchi na kuwa taasisi hizo zinapaswa kufanya kazi kama timu..
Mjumbe wa kamati hiyo, Mhandisi Isack Kamwelwe akisisitiza jambo katika ziara hiyo. |
Post A Comment: