DODOMA; WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Igunga mkoani Tabora, Athuman Msabila.
Awali, Msabila alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Akizungumza Bungeni leo Novemba 4, 2023 jijini Dodoma wakati uchangiaji wa hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma (PIC) Mchengerwa amesema kuanzia leo amemfuta kazi Mkurugenzi huyo.
Pia, amemuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi Adolf Nduguru kuwasimamisha kazi watumishi wawili wa wizara hiyo Aidhan Mpozi na Tumsifu Kachira kuanzia leo.
Mchengerwa amechukua hatua hiyo baada ya kupokea taarifa ya timu ya uchunguzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kuhusu mtandao wa upotevu wa fedha za umma kupitia mfumo mzima wa utoaji fedha kutoka Hazina kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Kamati imethibitisha pasipo shaka kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Athumani Msabila na maafisa tajwa wa Tamisemi wamehusika na upotevu wa fedha za umma” amesema Mchengerwa.
Aidha, amemuelekeza Mkurugenzi wa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kumsimamisha kazi Mwekahazina wa halmashauri hiyo Kabwengwe Nteminyanda kwa tuhuma za ubadhilifu wakati akifanya kazi kwenye halmashauri ya wilaya ya Kankonko na Uvinza mkoani Kigoma.
Pia, amewaelekeza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa wanaingia kwenye vikao vya Kamati ya Fedha vya Halmashauri bila kukaimisha na ambaye hatoingia vikao vya Kamati hiyo mara mbili mfululizo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Post A Comment: