Julieth Ngarabali, Kibaha.
Vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na matatizo ya uzazi vimepungua kutoka vitano kwa mwaka 2021 hadi vitatu kwa mwaka huu katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi na kwamba lengo ni kutokuwa na kifo kwa kipindi kijacho.
Takwimu hizo imeelezwa ni sehemu ya mafanikio ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau ya kupunguza kabisa ama kufuta vifo vya uzazi kwani hospitali hiyo inapokea wajawazito 2,400 kwa mwaka sawa na 200 kwa mwezi katika wodi ya wazazi idadi ambayo ni kubwa na inahitaji miundombinu ya kutosha na vifaa.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mbio za Coast City Marathon kwa niaba ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema Serikali imekuwa ikipambana na vifo vya mama na mtoto na changamoto zilizopo ambapo Wizara ya afya imeendelea kupambana nazo kuhakikisha zinaisha na huduma zinaboreshwa.
Lengo la mbio hizo za Coast City Marathon huko Kibaha Mkoani Pwani ni kutafutia fedha za kuchangia ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi kwenye hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata sh. 240 miliom zinazohitaji kwa ujenzi wa wodi ya wazazi.
Awali Mganga mkuu wa hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Dk. Amani Malima amesema mbio hizo ni kampeni ya kukusanya fedha kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo taasisi binafsi na serikali.
"Ni kweli jengo la wodi ya wazazi kwa sasa limeelemewa na wagonjwa na kulazimika kuomba msaada wa jengo lingine ambalo linasaidia kuhudumia wangonjwa wengi kwa wakati mmoja na kwamba ili kujenga jengo jipya sh. 240 Milioni kinahitaji na ndio maana wameamua kuzitafuta kupitia mbio hizo
Dk. Malima amesema hospitali ya Tumbi kwa sasa inapokea wagonjwa 500 kwa siku na 2,081 kwa mwezi na wanatoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa huo.
Aidha ameongeza kuwa Tumbi sasa inatoa huduma bora za matibabu zikiwemo za kuchuja figo, vipimo vya CT- Scan na inatoa ujuzi kwa wataalam wa afya na wajawazito mara kwa mara ili kuondoa kabisa vifo vitokanavyo na uzazi
Amesema hospitali ya Rufaa ya Tumbi ilipewa hadhi ya kuwa rufaa mwaka 2011 na inahudumia wagonjwa kutoka wilaya sita za mkoa huo na mikoa jirani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro.
" Lakini pia jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi,serikali inaendelea kushirikisha wadau mbalimbali ili kuchangia ujenzi wa miundombinu na vifaa tiba,”amesema.
Naye Mratibu wa mbio hizo za Coast City Marathon Dk. Frank Muhamba amesema wameanzisha kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi wa wodi ya mama na mtoto ambapo katika harambee taasisi na mashirika mbalimbali zimeshiriki michango ya fedha na vifaa vya ujenzi.
Katika siku ya kwanza ya ufunguzi mbio hizo zaidi ya sh 10 milioni zimepatikana kwenye mbio za Coast City Marathon kati yake sh. 5 Milioni imeahidiwa kutolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Baadhii ya wakina mama mjini Kibaha wamesema huduma kwenye wodi ya wazazi imeboreshwa kwani kuanzia Novemba 09 wajawazito wameanza kupata maji ya moto wodini.
" Tunashukuru namna Serikalini inavyotukumbuka wajawazito maana jumanne nilienda kumuona jirani yangu Gwantwa aliyejifungua akatuambia wanajikanda weyewe pale pale wodini maji ya moto yanatoka ,nilifurahi kwa kweli maana inatuvutia kupenda kuoga na kua wasafi mda wote kwa kweli"amesema Ester Mori
Post A Comment: