Mkurugenzi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Mhandisi. Exaudi Fatael,akizungumza leo Novemba 15,2023 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Watendaji wa Mamlaka za Maji nchini.
Baadhi ya Watendaji kutoka Mamlaka za maji za Mikoa na Miradi ya kitaifa nchini, wakifuatilia mkutano huo kwa makini uliofanyika leo Novemba 15,2023 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira EWURA, Mha. Exaudi Fatael (aliyekaa katikati) katika picha ya pamoja na Watendaji kutoka Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Mikoa na Miradi ya Kitaifa nchini, waliokaa kulia ni Mwakilishi kutoka Wizara ya Maji, Mha. Joviyus Mabula na Meneja Ufundi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira EWURA, Mha. Titus Safari (kushoto)
.................
Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imeziagiza Mamlaka za Maji za Mikoa na Miradi ya kitaifa kuwasilisha EWURA taarifa sahihi za utendaji kwa maendeleo ya sekta ya maji na taifa kwa ujumla.
Maagizo hayo yametolewa leo Novemba 15,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Mhandisi. Exaudi Fatael, wakati akifungua Mkutano wa Watendaji wa Mamlaka za Maji nchini.
Mhandisi. Fatael, amesema EWURA imebaini uwepo wa baadhi ya takwimu zisizo sahihi kutoka mamlaka za Maji, hivyo imeitisha kikao hicho maalumu ili kuhakiki usahihi wa taarifa hizo.
“Takwimu hizi zinatumika kuandaa taarifa ya tathmini ya utendaji wa mamlaka za maji kwa mwaka 2022/23, hivyo ni vema kuhakikisha maboresho ya takwimu hizi yanaakisi uhalisia wa utendaji wenu.”amesema Mhandisi Fatael
Ameeleza kuwa baadhi ya takwimu zinazoboreshwa ni pamoja na takwimu za kiwango cha maji yanayozalishwa, muda wa huduma, usafi wa mazingira na ubora wa maji.
Naye Mhandisi. Joviyus Mabula kutoka Wizara ya Maji,amezitaka mamlaka za maji kuhakikisha zinatoa takwimu sahihi kwani Wizara hutumia takwimu hizo kupanga mipango ya sekta maji.
EWURA huandaa taarifa ya tathmini ya utendaji wa mamlaka za maji nchini kila mwaka kwa mujibu wa kifungu cha 29(2) cha Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira.
Post A Comment: