Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Star Entrepreneur General kwa ufadhili wa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Mhe Aysharose Mattembe, limetoa mafunzo kwa wajasiriamali katika wilaya zote za mkoa huu ya namna ya kuendesha biashara zao kwa ufanisi na weledi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mafunzo hayo ambayo yalianza Oktoba 3, 2023 yalihitimishwa juzi Novemba 17, 2023 kwa awamu ya kwanza na yatakuwa endelevu ambapo kati awamu hiyo ya kwanza wajasiriamali walionufaika na mafunzo hayo ni zaidi ya wajasiliamali 1500 na ni kutoka Halmashauri za Wilaya Manyoni, Itigi, Mkalama,Iramba,Ikungi,Singida DC na Manispaa ya Singida.
Meneja wa shirika hilo,Yoel Mwenda akitoa taarifa wakati wa kufunga mafunzo hayo alisema wajasiriamali walifundishwa ufugaji wa kuku, kilimo biashara, usimamizi wa biashara, usindikaji wa mazao ya nafaka, mbogamboga na matunda pamoja na utengenezaji wa sabuni, za miche, utengenezaji wa Batiki, kujitangaza na utafutaji wa masoko.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo aliziomba halmashauri zote mkoani Singida kutoa kipaumbele cha kuwapatia mikopo ya kuendeshea biashara zao wajasiriamali waliopata mafunzo ya ujasiriamali.
Mattembe alisema pia atafanya utaratibu wa kuonana na taasisi zingine za fedha zinazotoa mikopo ili kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali ili waweze kukuza biashara zao na kujikwamua na umaskini na hatimaye kupiga hatua moja kwenda nyingine
Alisema, ‘’nataka kuona mwanamke wa Singida anayepika mandazi na vitumbua anamiliki kiwanda cha kuokea mikate, nataka kuona wanawake wa Singida wakimiliki migahawa mikubwa na wakimiliki viwanda vikubwa vya kukamua mafuta ya alizeti, inawezekana kabisa!’’
Mattembe aliongeza kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu na kila mwaka yatakuwa yakifanyika katika wilaya zote lengo likiwa ni kuungamkono jitihada za mhe Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kuona kila mtanzania anakuwa na shughuli ya kujiongezea kipato.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida, Naima Chondo ambaye alimwakilisha Naibu Waziri wa Maendeleoa ya Jamii ambaye alikuwa mgeni rasmi, akifunga mafunzo hayo alisema mafunzo hayo ni ya muhimu sana hasa katika wakati huu ambao serikali inawekeza kwenye viwanda na wajasiriamali.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa wanawake katika kukuza uchumi wa mtu mmoja, jamii na taifa ameondoa riba katika mikopo wanayokopeshwa wanawake kwa ajili ya kuanzisha shughuli za ujasiriamali.
Chondo aliwaahidi wajasiriamali hao kuwa atasimama kidete kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya kuhahikisha wajasiriamali hao wanapata mikopo inayotolewa na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa kusaidiana na Afisa Maendeleo ya Jamii.
Washiriki wa mafunzo hayo walimshuru Mbunge Mattembe kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yamewapa mbinu na stadi za maisha.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo lakiserikali Star Entrepreneur General lenye makao yake makuu mkoani Morogoro., Danford Kasaga akiwakabidhi keki iliyotengenezwa wakati wa mafunzo hayo kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na madiwani walioshiriki kupata mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa kwenye hafla ya kufunga mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo lakiserikali Star Entrepreneur General lenye makao yake makuu mkoani Morogoro., Danford Kasaga, akielezea jambo wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.
Mbunge Mattembe akiwakabidhi vyeti washiriki wa mafunzo hayo.
Mjasiriamali Neema Bahali kutoka Kijiji cha Nyuki, akikabidhi zawadi kwa mgeni rasmi na Mbunge Aysharose Mattembe.
Post A Comment: