Madiwani wa Halmashauri hiyo wamemuagiza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Gracian Max Makota asimamishe shughuli zote zinazoendelea katika maeneo ya Light In Africa na eneo la kujenga mahakama Mirerani hadi mgogoro uliopo utatuliwe.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer amesema maneno yanayosemwa kuwa baadhi ya waliokuwa viongozi wa CCM wamepora maeneo hayo na sasa wanauza rejareja kwa watu inabidi yafuatiliwe ili yakomeshwe.
"Inasemekana kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Simanjiro, ndugu Awadhi Omary amepora eneo hilo hivyo kusababisha kukosekana sehemu ya kujengwa mahakama na kituo cha afya hili jambo lifuatiliwe," amesema Taiko.
Diwani wa kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer amesema ni vyema mgogoro huo ukafikia tamati ili shughuli za maendeleo zifanyike kwa manufaa ya wananchi wa Mirerani.
"Halmashauri iliunda kamati ya kufuatilia mgogoro huo na kubaini madudu mengi kwenye ardhi hiyo hivyo ni vyema hatua zichukuliwe ili ujenzi wa taasisi za maendeleo zijengwe," amesema.
Diwani wa kata ya Ngorika, Albert Msole amesema ni vyema mgogoro huo wa ardhi ukafika mwisho kwani madiwani walishaelekeza kuwa waliosababisha hayo wachukuliwe hatua.
"Kama ni wenyeviti wa vitongoji wamehusika wachukuliwe hatua na kama ni viongozi kupitia CCM wamehusika chama kipewe taarifa wachukuliwe hatua nao," amesema.
Afisa ardhi wa Halmashauri hiyo Baltazary Sulle amesema watafuatilia suala hilo kwa kuhakiki nyaraka za wote wanaodai eneo hilo.
"Tutachunguza nyaraka hizo ili kubaini uhalali wake kwani hatutakubali kumuona mtu anaingia kwenye eneo hilo bila kuwa na vidhibitisho kwamba ni vya kwake," amesema Sulle.
Hata hivyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Awadhi Omary amesema eneo lake lipo mbali na sehemu hiyo iliyokuwa inamilikiwa na shirika la Light In Africa.
"Eneo langu nimelipata bila kutumia nafasi nilizokuwa nazo za Mwenyekiti wa CCM, diwani wa kata ya Mirerani na Mwenyekiti wa kijiji cha Mirerani" amesema Omary.
Post A Comment: