Na John Walter-Babati
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Babati wamepongezwa kwa kutekeleza miradi ya maji vijijini kwa weledi na kutatua kero ya upatikanaji huduma hiyo katika maeneo mengi ya wilaya hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara katika baraza maalum lililolenga kuwasilisha kero za wananchi kwa viongozi wa Taasisi za Serikali RUWASA, TANESCO na TARURA na kupatiwa majibu, kikao kilichohudhuriwa pia na mkuu wa wilaya Lazaro Twange.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Babati John Noya amesema wamekuwa wakipatiwa ushirikiano na viongozi wa RUWASA na kupatiwa majibu yanayoridhisha pindi panapokuwa na changamoto.
Diwani wa kata ya Boay Samson Shamba amebainisha kuwa RUWASA imetekeleza mradi wa maji unaowahudumia wananchi wa kata hiyo ambao walikuwa wakichota maji kwenye mitaro, na kutimiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua ndoo mama kichwani.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Babati Mhandisi Felix Mollel ameeleza kuwa wataendelea kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi kwa kuwa ndo msingi wa kuanzishwa taasisi hiyo kuhakikisha wanafikisha huduma ya maji safi salama kwa wakazi wa vijijini na kuhakikisha miradi ya maji yote inayotekelezwa katika maeneo hayo inakuwa endelevu ili kuwanufaisha wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amezitaka taasisi za Umma kushirikiana na madiwani katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Post A Comment: