Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ina jukumu nyeti la kusanifu na kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili iweze kutoa huduma kwa umma kwa haraka na ufanisi.
Mhe.Kikwete ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea Ofisi za eGA-Kituo cha Iringa ili kukagua utendaji kazi wa Mamlaka katika kituo hicho ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo.
“Dunia inakwenda kasi na teknolojia ni kila kitu kwa sasa, hivyo ni muhimu kwa eGA kufanya utafiti, kubuni na kutengeneza mifumo ya TEHAMA Serikalini kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma” amesema Mhe. Kikwete.
Mhe. Kikwete ameongeza kuwa eGA imeweka juhudi kubwa katika kusimamia TEHAMA Serikalini na imetengeneza na inaendelea kutengeneza mifumo ya TEHAMA ambayo imewarahisishia wananchi kupata huduma kwa haraka, mahali popote na kwa gharama nafuu na kuchagiza utawala bora.
Aidha, Mhe. Kikwete ameridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao katika ofisi zake zilizopo Iringa na amewataka watumishi wa Mamlaka kwa jumla kuendelea kubuni Mifumo ya TEHAMA inayotatua changamoto zilizopo nchini pamoja na kuwa wazalendo kwa maslahi ya Taifa.
Vile vile, amewasisitiza eGA kuhakikisha mifumo inayotengenezwa na iliyopo inakuwa na uwezo wa kuwasiliana ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Eng. Benedict Ndomba amemshukuru Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa kutenga muda wake kutembelea kituo hicho cha Iringa na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyotoa
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wa Kituo cha Iringa ikiwa ni zaira yake ya kikazi mkoani humo
Post A Comment: