Na John Walter-Morogoro

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewakumbusha vijana kuendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kuzingatia ndilo kundi linaloongoza kwa maambukizi mapya nchini.

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Kisayansi kuhusu maadhimisho ya Siku ya UKIMWI kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Jenista Mhagama ambapo alisema Kongamano hilo litafanyika kwa siku mbili tarehe 27 hadi 28 Novemba, 2023 Mkoani Morogoro.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Mwakilishi Mkazi USAID, Wadau wa Maendeleo, Viongozi wa Mkoa wa Morogoro, Wajumbe wa Bodi ya ATF, Baraza la Watu Wanaoishi na VVU Nchini (NACOPHA), Watekelezaji wa Afua za Kudhibiti UKIMWI, Viongozi wa Vyama vya Siasa na Viongozi wa Dini ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kuelekea Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu. 

Aidha lengo kuu la Kongamano hilo la Kitaifa ni kutathimini mafanikio, changamoto na mweleko wa Taifa katika kutekeleza Lengo la kutokomeza UKIMWI nchini ifikapo mwaka 2030 pamoja na kutoa taarifa za kisayansi zitakazoboresha afua za masuala ya UKIMWI.

“Kama tunavyofahamu Kauli Mbiu ya mwaka huu ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo pia ni kauli mbiu ya Kongamano letu ni “JAMII IONGOZE KUTOKOMEZA UKIMWI”. Hakika Kauli mbiu hii imekuja wakati sahihi ambapo kama taifa tunahitaji kuihamasisha jamii kuwa mstari wa mbele kuweza kutoa mchango wake katika kufikia azma ya kutokomeza UKIMWI tukianza na kuzuia maambukizi mapya hasa kwa vijana wetu hasa wasischana ambao kwa mujibu wa Takwimu wana kiwango kikubwa cha maambukizi mapya ya VVU,” alisema Naibu Waziri huyo.

Alitoa rai kwa jamii kuendelea kuchukua hatua na kupinga kwa nguvu zote masuala yote na tabia zinazochangia maambukizi mapya ikiwemo Unyanyapaa, Ukatili wa Kijinsi, Mila zinazochangia maambukizi, ngono katika umri mdogo, kuporomoka kwa maadili na tabia nyinginezo hatarishi. 

Akizungumza kuhusu Mfuko wa ATF amesema Serikali itahakikisha inaendelea kuhamasisha wananchi na wadau ikiwemo sekta binafsi kuchangia mfuko huu muhimu na Serikali pia kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko huo na kutafuta vyanzo vya uhakika zaidi vya kutunisha mfuko. 

Pia Kongamano hilo liwezeshe kutumia maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu pamoja na mambo mengine kuweza kujadili kwa kina ni kwa jinsi gani kama taifa tunaweza kuwakinga vijana ambao tumeelezwa kuwa Kiwango cha maabukizi ni kikubwa miongoni mwao. 

Aliongezea kuwa ni muhimu kwa wadau na kila mmoja kushiriki katika mapambano haya kwa kuzingatia kuwa Udhibiti wa UKIMWI ni suala mtambuka linalohitaji ubia na ushiriki wa kila mmoja ili kufanikiwa. 

“Ni matumaini yangu wadau wetu mliopo hapa kutoka sekta mbalimbali za kijamii mtatoa mchango muhimu sana katika Kongamano hili na hivyo kutuwezesha kuboresha zaidi mikakati yetu ya kutokomeza UKIMWI hapa nchini na kutimiza malengo ya kongamano,” alisisitiza Mhe. Nderiananga

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima alipongeza jitihada zinazofanywa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Nchini, huku akiikumbusha jamii kuendelea kupinga masuala ya Unyanyapaa kwa WAVIU na kueleza kuwa, kuwa na Virusi vya UKIMWI siyo mwisho wa Maisha kwani yapo magonjwa mengi na hayana tiba ya kudumu, hivyo wenye maambukizi hayo kuendelea kutumia dawa za kufubaza makali vya VVU na kuzingatia ushauri wa madaktari.

“Kipekee nawapongeza TACAIDS kwa kuchagua kuadhimisha wiki hii Mkoani Morogoro, niitumie nafasi hii kuendelea kupinga vikali tabia ya unyanyapaa kwa wenzetu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwani wana haki sawa, wanapaswa kuheshimiwa na kupewa nafasi katika jamii,” alieleza Mhe Malima.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Jerome Kamwela alisema kuwa Tume itaendelea kutoa elimu kwa umma hususan kundi la vijana ili kuhakikisha kundi hili linafikiwa na kuwajengea ujasiri katika mapambano dhidi ya Virusi ya UKIMWI, huku akiwaasa kuendelea kupima afya zao ili kutokomeza maambukizi mapya.


Share To:

Post A Comment: