Julieth Ngarabali ,Pwani.
Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM ) Mkoa wa Pwani imeelekeza watumishi na wataalamu wa Serikali Mkoani humo kuhakikisha wanakamilisha miradi yote ambayo bado haijakamilika ifakapo Desemba mwishoni mwaka huu kwani fedha zake zilishatolewa na Serikali kuu.
Miradi hiyo ni pamoja na ya afya, Elimu na miundombinu,maji, umeme na barabara kwani Serikali ilishatoa fedha za ujenzi wake, lakini katika ziara iliofanywa na kamati ya siasa Mkoani humo imebainika bado haijakamilika kwa asilimia mia ni mingi imefikia asilimia 98 tu ya utekelezaji wake.
Maelekezo hayo yametolewa kwenye kikao cha Halmashauri kuu ya CCM cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa kipindi cha Machi 21 /2021 hadi Juni 2023 na kwamba wasilisho hilo lilipokelewa na wajumbe hao kwenye ukumbi wa mikutano ya shule ya Mwalimu Julius Nyerere Kwamfipa Kibaha.
"Tumefanya ziara kamati ya siasa katika Halmashauri zote kasoro Mafia na tumeona kuwa miradi hiyo imefikia asilimia 98 ya utekelezaji na sehemu zilizobakia ni ndogo sana ambazo ni za kumalizia tu hivyo tunaelekeza Desemba mwishoni iwe imekamilika kwa asilimia mia "amesema Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani Benard Ghaty
Amesema katika utekelezaji huo wameona mwenendo wake unaenda kwa ufanisi na kinachotakiwa ni kuendeleza ufanisi huo ili kwenda sawasawa na uhalisia wa pesa zilizotolewa na Serikali.
Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo kamisaa Abubakari Kunenge ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo amesema Mkoa huo ulipokea sh . 1.19 Trilion katika kipindi cha 2021/2022 na Januari/Juni 2023 kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kamati ya siasa imepita kukagua na kuona maendeleo ya ujenzi wake
" Katika kikao hiki sisi tumewasilisha taarifa ya miradi yote ambayo hata mingine kamati ya siasa haikuweza kupita na tumeamua kutumia utaratibu wa teknorojia ambapo hata maeneo ambako wajumbe hawakufika wameweza kuona kwa sababu tulichofanya sisi tumeeleza ibara inasema nini kwa sababu ukiangalia Ilani imetoa maelekezo yaliyo mahususi na maelekezo yaliyo ya jumla hivyo tumesema kwa kila Idara Serikali imefanya nini"amesema.
Na kuongeza "tunamshukuru Rais kwakuwa mlezi mwema wa kutuongoza na kutufundisha namna ya kuhudumia wananchi na sisi kama wasaidizi wake kwa kushirikiana na watendaji wengine wakiwemo wabunge kwa sababu shughuli zilizofanyika bila kupitishwa kwa bajeti zisingetekelezeka"amesema Kunenge
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwishehe Mlao amesema ili kwenda na wakati kuna ulazima wana CCM kubadilika na kwenda na wakati kwa kuzingatia muda wa utekelezaji wa majukumu yao na hata kuhudhuria vikao
"Niwakumbushe wajumbe tusiendelee na zama zilizopita ni vema tukabadilika hususan katika kujali muda wa utekelezaji wa majukumu yetu na si kubaki na zama za karne zilizopita, kama ni saa fulan Kuna jambo hili tuzingatie muda " amesema
Awali baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kamati ya siasa ilitoa mapendekezo manne kwa wajumbe wa Halmashauri kuu ikiwemo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akielekeza fedha kwenye miradi mikubwa ikiwemo ya kimkakati mkoani Pwani
Mapendekezo mengine ni kumpongeza Mkuu wa Mkoa Kunenge kwa kusimamia utekelezaji wa miradi iliyokaguliwa, Viongozi wa CCM ngazi zote kwa kushirikiana na wataalamu kusimamia miradi hiyo na kutaka ipokee wasilisho hilo na itoe nguvu kwa watendaji wa Serikali kukamilisha pale ambapo mingine hawajakamilisha.
Ikumbukwe kwamba Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa ya kimkakati ambapo baadhi ya miradi inayotekelezwa ni pamoja na wa umeme kutoka bwawa la Mwalimu Nyerere na barabara ya njia ya nne ya Kimara/Kibaha
Post A Comment: