Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt.Wilson Mahela awataka wafamasia pamoja na waganga wakuu wa mikoa kwenda kusimamia vizuri upatikanaji na matumizi sahihi ya bidhaa za afya.
Dkt.Mahela ameyasema hayo leo jijini Dodoma, wakati akifunga kikao kazi cha wafamasia pamoja na waganga wakuu wa mikoa kilicholenga kujadili utekelezaji wa mpango wa IMPACT unaolenga kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
‘’Nendeni mkahakikishe shughuli za usimamizi wa bidhaa za afya unakuwa mzuri kwenye ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za afya.Tunataka tuone huduma bora za afya zinazoendana na upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba.Nendeni mkaweke takwimu zote za dawa na vifaa tiba ili ifahamike bidhaa zilizopokelewa na bidhaa zilizotumika,” amesema.
Dkt.Mahela ameongeza mikoa na halmashauri ikahakikishe kazi za usimamizi shirikishi zinafanywa kwa ushirikishwaji wa waratibu wote wakiwemo wafamasia ili kuhakikisha swala la bidhaa za afya linaboreshwa kwenye miradi yote .
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Afya Ustawi wa jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt.Rashid Mfaume amewaagiza waganga wakuu wa mikoa pamoja na wafamasia walioshiriki kikao hicho kuhakikisha wanakomesha tabia ya wizi wa bidhaa za afya ambao unaleta sifa mbaya kwa kada ya afya na kuiletea hasara serikali.
Post A Comment: