Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amemuagiza Afisa Madini Mkazi Mkoa wa kimadini wa Mbogwe kuandaa na kuratibu mkutano kati ya Wachimbaji Wadogo wa Mbogwe na taasisi za kifedha ili wapate elimu kuhusu mikopo inayotolewa na taasisi hizo na hatimaye kukuza mitaji yao.
Ametoa rai hayo, leo Novemba 14, 2023 wilayani Mbogwe mkoani Geita wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa Mbogwe katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mgodi wa Isanjabadugu & Partners Nyakafuru wilayani humo.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapiga hatua na kufikia kuwa wachimbaji wa kati na wakubwa siku za usoni na kwamba ili wapige hatua kufikia malengo hayo wanahitaji kufahamu namna wanavyoweza kupata mikopo kwasababu tayari taasisi za kifedha zimekubaliana na Serikali kuhusu kuwakopesha wachimbaji hao.
“Nikuelekeze Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huu wa kimadini, tenga siku uandae mkutano kama huu, ziite taasisi za kifedha zije ziwaeleze wachimbaji hawa namna ya kupata mikopo nafuu ili waongeze mitaji yao. Masharti ya benki ni mawili, kwanza ni taarifa ya uzalishaji ya mgodi husika na pili ni taarifa ya kijiolojia ya eneo hilo lenye leseni, hapa tunafahamu kuwa utafiti bado ni duni, ila Wizara kupitia taasisi zake itakuja kufanya utafiti zaidi hapa ili tupate taarifa za kina za kijiolojia” amesema Dkt. Kiruswa.
Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sakina Mohamed alimuomba Naibu Waziri Dkt. Kiruswa kupitia Wizara kuwatafutia wawekezaji wakubwa wa madini kwa kuwa wilaya hiyo haina mwekezaji wa aina hiyo hata mmoja jambo linalopelekea kutegemea wachimbaji wadogo pekee katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika Sekta ya Madini pamoja na ukarabati wa miundombinu ya huduma za kijamii katika wilaya hiyo.
Akitolea ufafanuzi maombi hayo, Dkt. Kiruswa ameitaka wilaya hiyo kutumia fursa za maonesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa kushiriki na kutangaza fursa hiyo ya uwekezaji katika rasilimali madini huku akiwaahidi kuwa balozi wa wilaya hiyo kuinadi fursa za madini ndani na nje ya nchi kupitia making makongamano atakayokuwa akialikwa na kushiriki.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe, Ernest Maganga amesema kuwa amepokea na anafanyia kazi maelekezo ya Naibu Waziri Dkt. Kiruswa kwa kuandaa ratiba ya kuwatunanisha wachimbaji wa mkoa huo wa kimadini na taasisi za kifedha ili kutatua changamoto ya mitaji sambamba na kuwaelimisha kuhusu utaratibu wa kukopa benki.
Akizungumza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali tangu kuanzishwakwa Mkoa huo wa kimadini, Maganga amesema mwaka wa fedha wa 2021/2022 Mkoa huo ulikusanya asilimia 99.5 ya lengo la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali ambako shilingi bilioni 21.39 zilikusanywa kati ya lengo la bilioni 21.5 wakati kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, Mkoa huo wa kimadini ulipangiwa kukusanya shilingi bilioni 32.09 ambako zaidi ya shilingi 22.43 zilikusanywa kiasi ambacho ni sawa na asilimia 69.8 ya lengo.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha wa 2023/2024, Mkoa huo umepangiwa kukusanya shilingi bilioni 35 ambako kwa kipindi cha mwezi Julai hado Oktoba 2023, kiasi cha shilingi bilioni 10.7 zimekusanywa sawa na asilimia 30.6 ya lengo la mwaka mzima.
Post A Comment: