Mkuu wa Dawati la Jinsia wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, Mkaguzi wa Polisi Amina Abdallah, ambaye alikuwa mgeni rasmi akizungumza na Wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakati akizindua rasmi dawati la jinsia Oktoba 1, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
JESHI la Polisi Mkoa wa Singida limezindua rasmi dawati la jinsia katika
Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida kwa lengo la kukabiliana
na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa taasisi hiyo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Mkaguzi wa Polisi
Amina Abdallah ambaye alikuwa mgeni rasmi na kuongozana na Koplo Eva Julius wa
dawati hilo, akizungumza Novemba 1, 2023 kwenye uzinduzi huo alisema dawati
hilo litasaidia kwa wanafunzi wanaopatwa na madhira kutoa taarifa ili
changamoto zao ziweze kufanyiwa kazi.
Alisema viongozi wa dawati hilo ambao watakuwa wanapokea taarifa kabla ya
kuzifikisha ngazi za juu wazingatie suala la usiri ili wanafunzi waweze kuwa na
imani na dawati hilo.
Abdallah alipongeza uongozi wa taasisi hiyo kwa kazi nzuri ambayo imesaidia
kudhibiti vitendo vya unyanyasa wa kijinsia katika msimu wa masomo uliopita
hakujaripotiwa matukio ya unyanyasaji wa
kijinsia yakiwamo ya ubakaji na ulawiti ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
" Huu utaratibu wa kuwa na dawati la kijinsia usiishie katika taasisi
hii bali uenezwe katika vyuo vingine na shule za msingi kwa kutoa elimu ya
kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na hiyo ndio itakuwa njia nzuri ya
kukabiliana na matukio hayo," alisema Abdallah.
Katika kuhakikisha dawati hilo linapata nguvu kushughulikia changamoto za
unyanyasaji wa kijnsia kwa wanafunzi
walichaguliwa wajumbe watatu kusimamia ambao ni Waziri wa Afya kutoka Serikali
ya Wanafunzi ya taasisi hiyo, Ramla Mchomvu, Mkutubi Francis Majele na Mlezi wa
wanafunzi, Asia Hansy,
Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Flora Lemnge aliwataka wanafunzi hao
watakapokuwa na changamoto yoyote ya ukatili wa kijinsia kwenda kutoa taarifa
kwa wajumbe hao ambao ni wasiri na wanauzoefu mkubwa ambapo kwa wavulana
aliwataka kwenda kumuona Mkutubi Francis Majele.
Mshauri wa wanafunzi katika taasisi hiyo, Ambwene Kajula alisema wanafuraha
kulizindua dawati hilo licha ya kuwa nalo na kuwa lengo la kulizindua ni kutaka
kuukataa na kuutokomeza kabisa ukatili katika jamii yao na watu wawe bora kama
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alivyoamua kuweka Wizara ya Ustawi wa Jamii na
kuona kazi ya dawati la jinsia lina msaada mkubwa.
"Dawati la jinsia linasaidia kuweka mazingira bora kwa wanafunzi na
kama wataweza kuongea na kupata sehemu ya kusema madhira yao walioyapata kwa
ukaribu tena kwa mtu ambaye amemzoea ni jambo jema sana," alisema Kajula.
Alisema katika kampasi hiyo wamechaguliwa baadhi ya walimu na watumishi kuwa wajumbe wa dawati
hilo ambao watasaidia kupokea taarifa kutoka kwa waathirika na kuzifanyia kazi
na kuyafikia malengo ya kutokomeza ukatili katika taasisi hiyo na nchi kwa
ujumla.
Mwanafunzi wa taasisi hiyo anayesomea ngazi ya cheti, Pendo Maube
akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema kupitia uzinduzi huo wameweza kujua
fursa mbalimbali ambazo zinapatikana katika dawati hilo la kijinsia kama kujua
haki zao na namna ya utoaji wa taarifa pale panapotokea changamoto ya ukatili
wa kijinsia.
Katika uzinduzi huo elimu mbalimbali zilitolewa ambapo Mkaguzi wa Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida , Mwantumu Bakari akiongozana na wataalamu wa jeshi hilo walitoa mafunzo ya
kukabiliana na majanga ya moto ambapo walitoa namba ya kutoa taarifa iwapo
kutatokea changamoto hiyo kwa kupiga namba 114.
Aidha, viongozi mbalimbali wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii
(SMAUJATA) mkoani hapa nao walipata fursa ya kutoa elimu ya kupinga vitendo
vyote vya ukatili na walitoa namba 116 ya kupiga kwa ajili ya kutoa taarifa za
vitendo vya ukatili ambapo wanafunzi hao walikubali kuwa mashujaa wa Smaujata.
Mbali ya elimu hiyo kutolewa na makundi hayo pia baadhi ya wawakilishi wa taasisi za kifedha kama benki ya NMB, CRDB na nyingine nao walitoa elimu ya namna ya utunzaji wa fedha ambapo walielezea umuhimu kwa wanafunzi hao wa kufungua akaunti ili kutunza fedha zao badala ya kuwa nazo kwenye mabegi na kukosa usalama.
Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Mratibu wa Taaluma, Flora Lemnge
akizungumza katika uzinduzi huo.
Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida , Mwantumu Bakari,
akitoa elimu ya jinsi ya kukabiliana na majanga ya moto.
Mshauri wa Wanafunzi katika taasisi hiyo, Ambwene Kajula, akizungumza
kwenye uzinduzi huo.
Naibu Smaujata Mkoa wa Singida, Kabelwa Ramadhani akizungumza na wanafunzi
wa TIA Kampasi ya Singida.
Afisa Kumbukumbu na Nyaraka wa TIA Singida, Juma Kihiyo akizungumzia jinsi
mwanafunzi anavyotakiwa kuomba ruhusa ya kutoka chuoni.
Katibu Gavana wa Wilaya ya Singida, Miraji Hamisi, akizungumza.
Katibu Idara ya Wanawake Smaujata Mkoa wa Singida, Evelyne Lyimo,
akichangia jambo kwenye uzinduzi huo.
Makamu Mwenyekiti Idara ya Wanawake Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Mkoa
wa Singida, Hapiness Francis akichangia jambo wakati akitoa elimu kuhusu
ukatili wa kijinsia na mambo mengine.
Mwenyekiti wa Smaujata Manispaa ya Singida,
Elineema Babu, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Elimu ya kukabiliana na majanga ya moto ikitolewa
na Afisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Wanafunzi wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi ukiendelea.
Wanafunzi wakishiriki uzinduzi huo.
Saluti ikipigwa wakati wimbo wa taifa ukiimbwa.
Mwenyekiti Idara ya Vijana Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii
(SMAUJATA) Manispaa ya Singida, Omari Mwangi, akitoa nasaha zake kwa wanafunzi
wa kampasi hiyo.
Shujaa mtoto wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii ambaye hakupenda kutaja jina
lake naye alikuwepo kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi huo ukiendelea.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi
Mgeni rasmi wa uzinduzi huo, Mkaguzi wa Polisi,
Amina Abdallah (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa dawati la
jinsia Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.Kutoka kushoto ni Ambwene
Kajula, Ramla Mchomvu, Asia Hansy na Francis Masele.
Muonekano wa moja ya gari la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambalo linatumika
kuzima moto.
Post A Comment: