NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Kukamilika kwa Mradi wa maji wa Kiburubutu unaoghalimu Shilingi Bil. 42 unatarajiwa kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Mji wa Ifakara.
Mradi huo unaotekelezwa na kusimamiwa na Wizara ya Maji chini ya Mkandarasi Mshauri (Consultant) WAPCOS LIMITED INDIA na Mkandarasi Mjenzi (Contractor) Larsen &Toubro Limited India, umefikia asilimia 7 ya ujenzi wake.
Akizungumza alipotembelea mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima
amesema mpango wa serikali ni kuhakikisha wananchi wamepata maji safi na salama bila ya kujali wapo mjini au kijijini.
"Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu, kukamilika kwake utasaidia upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama pamoja na kuchochea maendeleo kwa wakazi wa Mji wa Ifakara". Alisema Rc Malima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji na Mamlaka ya maji Safi na usafi wa Mazingira Ifakara (IFAUWASA) Mhandisi Ahmad Mpambaike amesema Mradi wa maji Kiburubutu unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2025 na utagharimu fedha kiasi cha shilingi Bilioni 42
Amesema kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji safi na salama ni asilimia 34 katika Mji wa Ifakara na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutamaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji na kufikia adhima ya serikali ya kumtua ndoa mama kichwani.
Post A Comment: