1000387825

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameitaka Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kutokafanya kazi za maofisi na badala yake kutembelea na kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi kuanzia ngazi za awali za manunuzi, mikataba, utekelezaji, ufanisi wa miradi kulingana na thamani ya fedha ili kubaini changamoto na kuishauri Serikali kwa wakati.

Agizo hilo amelitoa leo Tarehe 04 Novemba, 2023 jijini Dodoma wakati akizindua Bodi hiyo kutoka Taasisi mbalimbali nchini na kusisitiza kuwa ufumbuzi wa changamoto hiyo utasaidia kuokoa fedha ambazo hutolewa na Serikali katika matengenezo ya barabara hizo na kusaidia kuelekezwa katika kuongeza mtandao wa barabara nchini.

1000387830

Bashungwa ameagiza Bodi hiyo kufanyia kazi na kulipa uzito suala la kuharibika kwa barabara kipindi cha muda mfupi mara baada ya ujenzi kukamilika na kukabidhiwa Serikalini (Pre - Mature failure).

“Tunajenga barabara kwa mabilioni ya pesa, Mwaka mmoja barabara inakuwa kwenye uangalizi, baada ya hapo mkandarasi anakabidhi, Halafu baada ya hapo unakuta barabara inatakiwa ikae miaka 20, Mwaka wa tatu au wa nne barabara imeanza kuwa mbovu hivyo naomba mlipokee na mlifanyie kazi kwa uzito mkubwa, mkiwa wafanisi katika kulifanyia kazi hili tutaokoa mabilioni ya fedha za Watanzania”, amesema Bashungwa.

Ameitaka Bodi hiyo kutafuta mwarobaini wa suala la ongezeko la gharama za ujenzi wa miradi nje ya mikataba (variation) kwa kuwa suala hilo limekuwa Donda Sugu kwa Wakala huo na hivyo kusabababisha Serikali kuingia gharama kubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara nchini.

Aidha, Bashungwa ameiagiza Bodi kuangalia mkakati wa kuwasaidia wakandarasi wazawa bila kuathiri viwango vya majenzi ikiwemo kukaa na kuzungumza nao ili kujadili na kusikikiza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.

Kadhalika, Bashungwa amesisitiza Bodi hiyo kushughulikia suala la Rushwa kuanzia hatua za manunuzi, wakati wa kusaini mikataba pamoja na ukaguzi wa miradi ambapo amewataka kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakeyekiuka maadili ya kazi yake.

Ameagiza Bodi kuangalia namna ya kukiwezesha kitengo cha usimamizi wa miradi (TECU) kutoka TANROADS namna kukiwezesha ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na weledi katika masuala ya ushauri wa miradi ya barabara, Viwanja vya Ndege na madaraja wanayoisimamia nchini.

Waziri Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuifungua nchi kwa kwa kutoa fedha ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali inafanyika na kukamilika kwa wakati.

1000387829

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Amin Mcharo, ameahidi kusimamia majukumu ya Bodi kwa kutekeleza maagizo waliyopewa na Waziri huyo pamoja na kujifunza kupitia kwa Bodi zilizopita ili kuwatumikia wananchi.

1000387828

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour amesema Bodi hiyo ina wajumbe wasiozidi nane wanaoteuliwa na Mhe. Kwa mujibu wakifungu 9 (2)(b) cha Sheria ya Barabara ya mwaka 2007.

Amefafanua kuwa wajumbe hao wanatoka katika Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara ya Ujenzi, Bodi ya Mfuko wa Barabara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bodi ya Utalii Tanzania, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini na Shirikisho la Viwanda Tanzania.

Bodi ya Ushauri ya TANROADS inaundwa kwa mujibu wa kifungu 9 (2) (a-b) cha Sheria Na. 13 ya Barabara ya mwaka 2007 ambayo inaongozwa na Mwenyekiti anayeteuliwa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1000387826
1000387827
1000387831
1000387832
Share To:

Post A Comment: