Na Munir Shemweta, WANMM
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iko katika maboresho ya Sera ya Ardhi ili kuwa na sera itakayoleta suluhu kwenye changamoto za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kwa Taifa.
Hayo yamebainishwa tarehe 2 Septemba 2023 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.
‘’Tuko katika maboresho ambayo tunaendelea kuyafanyia kazi, na tutashirikisha wadau wengi sana kupata sera ambayo itaenda kutoa suluhu ya matatizo mengi ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi katika taifa letu’’ alisema Silaa.
Ametolea mfano wa moja ya maeneo yanayoenda kufanyiwa maboresho ni suala la umiliki ambapo amefafanua kuwa, mwananchi anapatiwa ardhi pasipo kuitumia huku sheria ya sasa ikiruhu kuimiliki bila ya kutumia.
Kwa mujibu wa Waziri Silaa, yeye na viongozi wenzake wa Wizara ya Ardhi wameanza mchakato mkubwa wa mabadiliko na kutaja moja ya mabadiliko ni kuondokana na ile dhana ya kila mtu anapokuwa na kipande cha ardhi basi lazima apime viwanja na kumilikisha ili watu wajenge nyumba.
‘’Tuje kwenye dhana ya kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi na tunapotengeneza mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi basi kuwe na mpango wa kutengeneza makazi ‘’ alisema
Aliweka wazi kuwa, Wizara yake itafanya maboresho mengi na moja ya maeneo itakayoangalia kwa makini ni pamoja na mabadiliko ya michoro ya matumizi, michoro ya upimaji na mipango miji na matumizi ya ardhi lengo likiwa kuangalia mabadiliko yanayofanyika kama yana faida na tija kwa taifa.
‘’Leo mtu inawezekana kabisa ameenda kununua ardhi akiamini kabisa eneo hili ni la makazi lakini baada ya muda mchache anakuta jirani yake amejenga shughuli ya biashara akiuliza anaambiwa sheria inatoa mamlaka kwa serikali kutoa mabadiliko ya matumizi ya ardhi lakni sheria hizi lazima zifuate msingi wa katiba’’ alisema
Akielezea zaidi kuhusiana na Siku ya Makazi Dunia, Waziri Silaa amesema, Wizara yake inaadhimisha siku ya Makazi Duniani kwa kufanya mjadala wa kitaaluma juu ya kauli mbiu ‘Uchumi himilivu wa miji – Miji kama kichocheo cha ukuaji na ufufuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa Silaa, madhumini makubwa ya Maadhimisho kwa mwaka huu ni kuwaweka pamoja wadau wa miji kujadili njia mbalimbali ambazo miji itatumia kurejesha uchumi baada ya Janga la Uviko 19 na kubadilishana uzoefu katika masuala ya mfumuko wa bei na changamoto za kifedha kimataifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda ametaka maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yawe na wiki maalum ya Makazi itakayokuwa na lengo la wizara kujitathmini na kuwapitisha wananchi kuelewa shughuli za wizara.
‘’Sisi kama wizara tumekosa siku ya kujitathmini naomba katika maadhimisho haya ya siku ya Makazi Duniani tuwe na wiki ya makazi ili tujitathmini na wakati mwingine tuwapitishe wananchi kuielewa wizara kwa sababu wakati mwingine inaweza kutoa mchango mkubwa lakini hauonekani’’ alisema.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema, wizara yake imefanya mambo mengi yanayohusiana na ardhi ikiwepo maendeleo ya makazi.
Hata hivyo, amesema kumekuwa na changamoto kadhaa hususan kwenye eneo la urasimishaji ambapo amebainisha kuwa, baada ya kufanya tathmini wizara imeona eneo hilo linahitaji kuwekewa nguvu kubwa na kutoa wito kwa watumishi wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanatekeleza mambo yaliyopangwa hasa ikizingaitiwa mipango ipo na mizuri.
Mwezi Disemba mwaka 1985 Baraza la Umoja wa Mataifa, kupitia Azimio Na. 40/202 liliazimia kuwa kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba kila mwaka itakuwa ni siku maalum ya kuadhimisha masuala ya makazi duniani. Siku hiyo hujulikana kote duniani kama Siku ya Makazi Duniani.
Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa chini ya uratibu wa Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT) huadhimisha siku hii kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafakari hali ya makazi katika nchi na changamoto zake husika na kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo. Leo, tarehe 2 ni Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba 2023, nchi yetu inajumuika na Jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani.
Post A Comment: