Na Shamimu Nyaki
Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imepokea taarifa ya Utekekezaji wa Majukumu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kulipongeza Baraza hilo kwa kuendelea kulea wasanii na kuwaelimisha pale inapotokea wamefanya makosa.
Akiwasilisha taarifa hiyo leo Oktoba 24, 2023 Jijini Dodoma,Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwijuma amesema hivi karibuni, Wizara kupitia Baraza hilo itazindua Muongozo wa kufanya kazi za Sanaa kwa Wadau wake ambao pamoja na mambo mengine utasaidia kufanya kazi za Sanaa zenye maadili yanayozingatia Utamaduni wa nchi,
"Sekta ya Sanaa imeendelea, mwaka 2022 imechangia asilimia 19 katika Pato la Taifa. Wizara itashirikiana na Wadau kufanya utafiti zaidi kuona Sekta hizo za burudani zinavyochangia katika Pato la Taifa kwa mwaka" amesema Mhe. Mwinjuma.
Amesema Baraza hilo linaendelea kufanya mapinduzi makubwa ambapo kwa sasa linatumia njia za kidijitali kusajili wasanii, kuanzisha BASATA VIBES, pamoja na Sanaa za mtaa kwa mtaa lengo likiwa ni kuwezesha vijana kupata nafasi ya kupata ajira.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mussa Sima ameagiza Wizara hiyo ifanyie kazi tathmini itakayoonesha mchanganuo wa namna Sekta hiyo inavyochangia katika Pato la Taifa huku akisisitiza maafisa Utamaduni nchini wasimamie vyema majukumu yao ya kukuza sanaa na kutoa elimu kwa Wadau hao juu ya namna wanavyoweza kunufaika Zaidi na kazi hiyo.
Wakichangia taarifa hiyo, Wajumbe wa Kamati hiyo wameishauri Serikali kusimamia vyema mapato ya wasanii, kuweka mazingira bora ya kufanya Sanaa, kusimamia maadili katika kazi za Sanaa na kuboresha kumbi zinazomilikiwa na Baraza hilo katika eneo la Sharifu Shamba Ilala jijini Dar es Salaam ili wasanii wapate eneo la kufanyia sanaa.
Post A Comment: