Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde  ameichambua  Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri  na kuinadi  kwa wadau  mbalimbali  wa Madini  zikiwemo Taasisi  za Umma na binafsi zinazojishughulisha na Sekta ya Fedha chini ya Mwamvuli wa Umoja wa Mabenki  Tanzania (TBA)   kwa kuonesha namna ilivyolenga kukuza uchumi na maisha ya Watu.

 Amesema Wizara imekutana na wadau hao  ili  kujadili  mchango wa Sekta ya fedha katika  kuinua Sekta ya Madini na kueleza kuwa, sekta hiyo inao mchango mkubwa wa kuiwezesha  sekta ya madini  kupiga hatua  kupitia utoaji mitaji na mikopo  ikiwemo kutengeneza  nafasi ya ushirikiano  ili kuimarisha zaidi  Sekta ya Madini nchini.

Ameeleza ikiwa kwa utafiti wa kina wa jiofizikia  wa urushaji wa ndege ( high resolution airborne Survey) umefanyika kwa  asilimia 16 tu  na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) umeiwezesha  sekta ya madini kupiga hatua kubwa kiuchumi ikiwemo kuchangia asilimia 56 ya thamani ya  bidhaa za madini zilizouzwa nje katika  Mwaka wa Fedha 2022/23, hivyo kufanyika kwa utafiti huo zaidi  utaongezea tija  zaidi.

 Akifafanua namna Sekta ya Madini inavyochangia kodi amesema imechangia  kodi za ndani kwa asilimia 15 ambazo ni  sawa na  Shilingi Trilioni 2 pamoja na kuchangia Dola za Marekani  Bilioni 3.3. kutokana na mauzo ya bidhaa  zinazotokana na rasilimali madini  kuongeza kuwa  ikiwa wizara  itawezesha kufanyika kwa utafiti wa angalau kufikia asilimia 50 ifikiapo mwaka 2030 kwa ushirikiano wa taasisi hizo,  tafiti hizo zitaliwezesha  taifa kupiga   hatua kubwa zaidi za  kimaendeleo na kiuchumi kupitia Sekta ya Madini.

 ‘’Tunataka kufahamu taarifa za miamba, ili tupumike vizuri, hii ndiyo sababu ya dira ya 2030. Ikifika 2030 tuwe tumefanya utafiti  kwa nchi yetu  kwa angalau asilimia 50.  Pamoja na mafanikio hayo bado machango wa sekta ya madini haujakidhi matarajio ya watanzania na taifa letu, zipo changamoto ndiyo sababu tumekutana kupitia kikao hiki kujadili kuwaonesha kilichopo kwenye sekta ya madini,  changamoto zilizopo na kutuondoa tulipo,’’ amesema Mhe. Mavunde.

Akizungumzia Madini  ni Maisha na utajiri  amesema  haviwezi kutenganishwa maisha ya mtanzania na Sekta ya Madini na kueleza kuwa kufanikiwa kwa tafiti za kina na kupatikana kwa taarifa za awali,  zitachochea sekta nyingine kukua ikiwemo Sekta ya maji na kilimo na kueleza, ‘kilimo wana mkakati wa kuchimba mabwawa 100, kupitia taarifa za GST inaweza kujulikana aina ya maji na hivyo  kufanya kilimo chake kwa tija na  kuwezesha  usalama wa chakula na mapato.

Kuhusu namna Sekta ya Madini inavyoweza kuokoa matumizi ya fedha za kigeni kwa  kununua mbolea  kutoka  nje, amesema zaidi ya tani 350,000  za mbolea  zinaagizwa nje  kwa kutumia fedha za kigeni  kwa ajili ya  matumizi ya  kupandia, kukuzia na kustawisha , hivyo, taarifa za miamba zitasaidia kujua  miamba yenye malighafi zenye mbolea inayohiajika na hivyo kusaidia shughuli za kilimo chenye  tija.

‘’ GST imewahi kufanya utafiti wa kina mwaka 2004   kwa kurushwa  ndege  katika maeneo ya  Kahama, Biharamulo, Nachingwea na Mpanda kwa ukubwa wa  kilomita za mraba 30,000  tu  ikilinganishwa na eneo la ukubwa wa nchi ya Tanzania yenye ukubwa wa kilomita za mraba  945,000 ni kiasi kidogo sana,  ndiyo sababu tumekutana na ninyi tuwaeleze fursa ziizopo kwenye Sekta ya Madini , tushirikiane,’’ amesema Waziri Mavunde.

Akizungumzia madini mkakati ameeleza  hivi sasa dunia imehamia kuzalisha nishati safi isiyochafua mazingira ambapo madini yanayohitajika  kuzalisha nishati hiyo ni pamoja na madini ya graphite, colbat, manganese, nikeli  na kueleza kuwa,  Tanzania  inayo nafasi kubwa ya kuwa mzalishaji wa madini hayo kwa kuwa yanapatikana nchini na kuongeza , ifikapo mwaka 2050 mahitaji ya madini hayo duniani yatafikia tani milioni 150.

 Kufuatia hali hiyo, amesema  Sekta ya Madini ni  sekta ambayo endapo itafungamanishwa  na sekta nyingine  itawezesha watu kupata mafanikio, tija, uwekezaji na maendeleo na kueleza  kuwa  Serikali  imedhamiria kutekeleza azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye utafiti wa   madini mkakati.

 Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse wakati akitoa wasilisho   amesisitiza kuwa uchimbaji mdogo ni eneo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee na taasisi za fedha na kueleza  kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi  Kisheria katika shughuli za uchimbaji mdogo  ikiwemo kuliwezesha Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA) kuwa na uwakilishi  Tume ya Madini, kuwatengea maeneo na kuwapatia elimu.

 Amezieleza changamoto za ukosefu wa masoko, teknolojia duni, kutokukopesheka, elimu, na kueleza kuwa, tayari STAMICO imechukua hatua kadhaa  ikiwemo  kuandaa mpango  kutoa elimu kwa kuzunguka nchi nzima,   kusaini  makubaliano na GST  kuwezesha  kupatikana kwa taarifa za kijilojia, kusaini hati za makubaliano na baadhi za benki ikiwemo CRDB, KCB na NMB  na kuelezakuwa, hayo yote yamefanyika ili kupunguza   hatari kwa taasisi za fedha na hivyo kuzitaka taasisi hizo kujenga imani na wachimbaji kwa kuwa tayari Serikali imeingilia kati ikiwemo kuwarasimisha.

Ametolea mfano wa   ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Australia, Down Under  na kueleza  namna nchi ya Tanzania ilivyokuwa kivutio katika mkutao huo  kwenye  madini mkakati na kueleza kuwa, taasisi za fedha zinapaswa kutumia fursa za mazingira ya ndani kuwawezesha wachimbaji wadogo kuweza kuchimba madini hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TBA  Theobas Sabi amesema  anaishukuru Wizara kwa mkutano  huo ambao umeziwezesha tasisi za fedha kuielewa Sekta ya Madini, pia amesema kutokuwepo kwa taarifa za  kujua kiasi cha madini kilicho kwenye leseni za wachimbaji ni eneo ambalo limekuwa  changamoto kwa mabenki na kueleza kuwa, taasisi hizo zitayachukua yaliyozungumzwa katika mkutano huo kwa ajili ya kuyajadili kwenye vikao kazi vya jumuiya hiyo.

Mbali na taasisi za fedha, wengine waliohudhuria kikao hicho  ni  pamoja na wafanyabiashara wa madini, watoa huduma, wahimbaji Wadogo, Wa kati Wakubwa. Aidha, wadau hao wamepongeza kwa hatua ya wizara kuitisha  kikao hicho.
Share To:

Post A Comment: