Na Sixmund Begashe
Wakazi Wilayani Lujewa Mkoani Mbeya wametakiwa kuitunza Miradi ya Umwagiliaji inayotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi wa Maliasili na ukuzaji wa Utalii Nyanda za juu Kusini (REGROW) kwemye eneo la Madibira na Mbarali kwa kuwa miradi hiyo ni kwa ajili ya wananchi wenyewe.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba alipotembelea na kukagua shughuli za ufukuaji wa mto Kioga, mto ambao ulikuwa umehama kwenye mkondo wake wa asili, ujenzi wa mifereji ya Umwagiliaji kwenye mashamba ya mpunga Madibira, Ujenzi wa Ofisi pamoja na kuongea na uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mahonga, Madibira.
Kamishna Wakulyamba ameongeza kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatekeleza Mradi wa REGROW kwa lengo la kuwainua wananchi kiuchumi kupitia uhifadhi wa Maliasili na Utalii, hivyo ni vyema wananchi wakawa mstari wa mbele katika kuhakikisha miundombinu inayojengwa inadumu na kuwanufaisha watanzania wote kwa ujumla.
Aidha Kamishna Wakulyamba licha ya kupongeza kwa usimamizi wa kazi nzuri inayoendelea, ameagiza wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha ujenzi na ufukuaji wa mifereji hiyo kwa wakati na ubora ili wakulima waendele kunufaika kiuchumi pamoja na ustawi wa Ikolojia na Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kupitia Mto Ruaha Mkuu.
Awali akitoa Taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa REGROW Wilayani Lujewa, Msimamizi wa Mradi huo Dkt. Aenea Saanya ameeleza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha Maji yanatiririka kwa wingi Mto Ruaha, kwa kuyadhibiti maji ambayo yalikuwa yakisababisha mafuriko kwenye makazi ya watu, na kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji katika kilimo cha umwagiliaji, na kuwa mradi wa Madibira hadi kukamilika utagharimu Shilingi Bilioni nane.
Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji cha Mahongo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw. Lukas Mathayo, ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwezesha utekelezaji wa REGROW katika eneo hilo, na kuahidi kuwa, serikali yake na wananchi kwa ujumla wataendelea kushirikiana vyema katika ulinzi wa miundombinu inayoendelea kujengwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Post A Comment: