Yese Tunuka,Kilimanjaro

Wananchi  wa  kijiji cha Lotima , Kata ya Makuyuni , Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka kuwajengea kivuko kinachounganisha baadhi ya vijiji katika kata hiyo kiwaepushe kusombwa na maji pindi wanapovuka kufuata huduma za kijamii nga'mbo ya pili. 

Wanafunzi wa Kijiji hicho wanaosoma shule ya Sekondari ya Himo wamekuwa ndiyo waathirika wakubwa ambapo wanalazimika kutembea umbali wa kilometa 7  kufuata elimu wakati wa mvua baada ya kivuko kilichokuwepo kusombwa na maji.

Wakizungumza na waandishi wa habari ,Wananchi hao  wameiomba serikali pamoja na viongozi wa chama kuangalia namna ya kuwawekea kivuko ili kiwanusuru wananchi  na watoto wao wanaosoma ng'ambo ya pili kuepuka  hatari ya kusombwa na maji pindi wanapovuka kufuata elimu mjini Himo. 

Abdu Musa , Mkazi wa kijiji hicho amesema kukosekana kwa kivuko hicho (daraja) imekuwa ni changamoto kubwa sana kwao huku wakihofia watoto wao kuvutwa na maji hasa katika kipindi hiki Cha mvua za Elinino.

"Tunaomba serikali itusaidie kutengeneza kivuko maana tunapata shida kila siku,Sasa hivi mvua zikinyesha wanafunzi kuvuka ni changamoto,mara nyingi wanakuwa hawaendi shule kwaajili ya mafuriko  wanaogopa  maporomoko ya maji maana korongo limezidi kumong'onyoka   na barabara hamna." 

Hamza Bakari ambaye pia ni mwananchi wa kijiji hicho ameiomba serikali kuangalia utaratibu wa kuwawekea angalau kivuko Cha dharura  ili kiwasidie  katika kipindi hiki ambacho mvua za Elinino zinatarajia kunyesha huku akiwataka Wazazi wawasidie watoto wao kuvuka hadi watakapofika barabara ya lami.

"Natoa tahadhari kwa wananchi wanaoishi ng'ambo ya pili ya Kitongoji Cha Kifula ,wazazi tuwasaidie watoto wetu hasa kipindi hiki cha mvua,pia tuwasiliane na Walimu maana wanafunzi watapewa adhabu kwa kuchelewa kwenda shule kwa wakati"

Naye Diwani wa kata ya Makuyuni,Mh. Dickson Tarimo amekiri kuwa ni kweli changamoto hiyo ipo kutokana na asili ya udongo wa eneo hilo ambapo humongonyoka pindi mvua zinaponyesha na kusababisha korongo kuwa kubwa ambapo ametanabaisha kuwa ameomba msaada kwa wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) kuwasaidia kutatua changamoto hiyo iliyosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.

"Sisi kama wananchi tutafanya tutakavyoweza chini ya  uangalizi wa  TARURA,watusaidie kama wataweza kutusapoti,kile kivuko kianze kutumika na Wananchi tena kwa muda,wakati serikali ikiendelea kujipanga kutatua hilo.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Kifula,Salim Mdee amesema "Tumewasiliana na wadau mbalimbali watusaidie wakati tukisubiri hilo ambapo mmoja ametuahidi atatupa reli ili tutengeneze kivuko Cha muda ili wakazi wa hapa pamoja na wanafunzi waweze kupita pale wakienda shule.

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: