Waziri wa Madini Mh.Anthony Mavunde amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia S. Hassan itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini na kwasasa wamejipanga kuwawezesha nguvu kazi ya vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini.
Waziri Mavunde ameyasema hayo jana wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya machimbo kusikiliza changamoto mbalimbali za wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Waziri Mavunde akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mh.Mayeka Simon Mayeka alipokelewa na wachimbaji zaidi ya 200 ambao katika mkutano walitaja changamoto zao mbalimbali kama vile ukosefu wa mitaji , vifaa duni vya uchimbaji , ukosefu wa Nishati ya Umeme na kukosekana kwa Miundombinu salama.
“Nianze kwa kuwatoa hofu wachimbaji kwa kuwaambia kuhusu mikakati mbalimbali iliyowekwa na Serikali kufuatia maelekezo ya Mh.Rais Dkt. Samia S. Hassan katika kuwainua wachimbaji wadogo nchi nzima kwa kuwapatia maeneo ya uchimbaji,mashine za uchorongaji,kuwaunganisha na Taasisi za fedha ili kupata mikopo yenye riba nafuu,kuwaunganisha na kampuni za uuzaji wa vifaa & mitambo ya uchimbaji sambamba na mpango wa kufanya utafiti wa kina ili kupata taarifa sahihi za miamba na madini.
Niwaombe vijana wote mliopo hapa kujikusanya na kujisajili katika vikundi rasmi ili iwe rahisi kuwafikia na kuwahudumia.
Ninamuagiza Afisa Madini Mkazi Chunya Ndg. Sabahi Nyansiri kusimamia na kuratibu zoezi hilo la kuunda vikundi na kuvisajili katika mifumo rasmi ili vitambulike na mamlaka husika”Alisema Mavunde
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mh. Mayeka S. Mayeka amesema uongozi wa Wilaya ya Chunya upo tayari kushirikiana na wizara,vyama vya wachimbaji na wadau wote kuhakikisha azma na lengo la kuwawezesha wachimbaji linatimia.
Post A Comment: