Viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wamehimizwa kutumia matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022 kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kwenye Jamii.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe. Kasilda Mgeni alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu wakati wa Ufunguzi wa semina ya usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa Viongozi, Watendaji na Wadau wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema mipango ya maendeleo izingatie Matokeo ya Sensa na mwenendo wa Kasi ya ongezeko la idadi ya watu katika Mkoa wa Kilimanjaro hasa katika utoaji wa huduma mbalimbali za Kijamii ikiwemo Elimu, Afya, Maji na Miundombinu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Tixon Nzunda amesema atasimamia mipango yote ya Mkoa na Bajeti inayokwenda kupangwa kwa mwaka wa Fedha ujao itazingatia takwimu halisi za Sensa katika maeneo yote ya Halmashauri Saba za Mkoa kwa kuzingatia mipango ya fursa na maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Aidha, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imewekeza katika sekta ya Afya hali inayopelekea Mtanzania anayezaliwa sasa umri wake wa kuishi hapa Duniani kuwa ni miaka 65 huku Mwananchi wa mkoa wa Kilimanjaro umri wake wa kuishi ukiwa ni miaka 63.
Amesema kuwa, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 1978 ilionyesha umri wa kuishi kwa Mtanzania ni miaka 44 ambapo hii yote imechangiwa na kiasi kikubwa na uwekezaji unaofanyika na Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya Afya.
Post A Comment: