Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, John Mwanja, akizungumza Oktoba 27, 2023 na wahitimu wa mafunzo ya Nishati ya Umeme Jua   yaliyoandaliwa na VETA kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC). Kulia ni Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka ATC, Daniel Ngwenya na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Singida, , Alphonsina James.

...............................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeanza kutoa elimu ya Nishati ya Umeme Jua katika vyuo vyake vyote nchini ikiwa ni moja ya njia ya kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassanza kuhakikisha nchi inapata umeme wa uhakika.

Akizungumza Oktoba 27, 2023 , wakati akifunga mafunzo ya nishati ya umeme jua ya wiki mbili kwa walimu wa vyuo 12 vya VETA ambayo yameandaliwa na VETA Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja alisema mafunzo hayo ni ya muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inamgawo wa umeme na inafikiria kuiwasha kwa kutumia umeme huo kupitia wataalamu waliozalishwa na VETA.

“VETA ndio tumepewa majukumu ya kutoa elimu hii kwenye vituo vyetu na kuhakikisha watanzania wote waliopo mijini na vijijini wanaipata,” alisema Mwanja.

Mwanja alisema kupitia wahitimu hao sasa VETA inakwenda kupata walimu wa kufundisha kozi hiyo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA aliwaomba wakuu wa vyuo katika kanda zao kuwaruhusu walimu kuhudhuria mafunzo hayo.

Alisema mafunzo hayo yalianzishwa VETA Mkoa wa Singida ambapo awamu ya kwanza na ya pili yamefanyika hapo na kwa awamu hii waliona yasihusishe watu wa kutoka Singida pekee bali uongezwe wigo wa kuwapata wengi lengo likiwa yasambae kila sehemu ambapo VETA ipo.

Alisema ilipendekezwa hivyo si kwa ajili ya kupata watu wengi bali viwepo vituo vingine kama cha Singida kwenye vyuo vingine kwa ajili ya kupata elimu na wataalam kwenye maeneo hayo.

Alisema kama inavyofahamika majukumu ya VETA ni kufundisha ujuzi na kuwa elimu hiyo ya nishati ya umeme jua ni muelekeo na mpango wa Serikali kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa ya umeme na kuwa moja ya maono ya Serikali ni kuona nchi inapata umeme kutokana na mfumo wa jua.

Alisema wanapotegemea kupata umeme kupitia mfumo huo ni lazima wawepo wataalam wa kutosha wa kufanya kazi hiyo na kuwa kuna wadau wengi kama Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ambao wanafundisha kozi hiyo lakini na VETA wanaowajibu wa kuiunga mkono Serikali wanapotaka kuongeza nishati hiyo kwa kuhakikisha wataalam wanapatikana.

“Haiwezekani wataalam hao wapatikane kwa kutumia kituo cha Singida peke yake hivyo VETA kama wajibu wetu ni lazima wataalam hao wasambae nchi nzima,” alisema Mwanja.

Alisema mahitaji ya VETA ni kutaka kijana aliyopo kule Busokelo mkoani Mbeya au Mwanza na maeneo mengine ya nchi wapate elimu hiyo katika vyuo vilivyopo katika maeneo yao badala ya kwenda Singida jambo litakalowapunguzia gharama na ndio maana Serikali inajenga vyuo vya VETA kila wilaya kwa lengo hilo na kuwa jukumu lao ni kupeleka huduma kwa watumiaji na wadau wao ambao ni hao wanafunzi.

Mwanja alisema kutokana na hali hiyo VETA iliona licha ya kozi hiyo kuanza kutolewa Mkoa wa Singida sasa itolewe katika Mikoa yote kupitia vyuo vya VETA ikiwa ni kuwasogezea huduma watanzania.

Aidha, Mwanja aliwataka wahitimu hao mara watakaporudi kwenye vituo vyao wakawe na mwendelezo wa kwenda kutoa elimu hiyo ambayo pia wanafunzi wanaojifunza fani ya umeme wa kawaida katika chuo hicho wameyapata.

Katika hatua nyingine Mwanja alivitaka vyuo hivyo kujitangaza ili shughuli wanazozifanya zifahamike ikiwa ni pamoja na mafunzo ya nishati ya umeme jua jambo litakalosaidia kufahamaika na akahimiza pia kuanzisha kozi fupi za mafunzo hayo.

“Suala la kujitangaza ni la muhimu tumieni mitandao ya kijamii kuna chuo kimoja kule Ruvuma nilikuta kuna raia wa kigeni kutoka nchi jirani ikiwemo Msumbiji wapo kupata mafunzo   nilipouliza walijueje kama kuna hicho chuo walisema kupitia matangazo hivyo ndugu zangu tangazeni vyuo vyetu kwani biashara ni matangazo,” alisema Mwanja.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Singida, Alphonsina James aliwashukuru washiriki wa mafunzo hayo kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha wakati wa mafunzo na kueleza kuwa kwao ni bahati kubwa kwani katika vyuo 48 ni vyuo 15 pekee ndio vilivyotoa washiriki hao.

Katika risala ya wahitimu hao kwa mgeni rasmi waliomba muda wa mafunzo uongezwe pamoja na uratibu wa mafunzo hayo ufanywe na VETA makao makuu kwa ajili ya uwezeshwaji ambapo pia waliomba kuwezeshwa vifaa vya kufundishia.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, John Mwanja, akikabidhi cheti kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo.

Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hutuba ya mgeni rasmi wakati wa ufungaji wa mafunzo.
Mgeni rasmi wa ufungaji wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, John Mwanja (waliokaa katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo hayo.


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: