Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema haki ni katika Mihimili Mikuu ya Amani, pindipo ikikosekana ni vigumu kuiongoza Nchi kwa Misingi ya Utawala Bora, na hatimaye ikawa siyo rahisi kuyafikia maendeleo.
Mheshimiwa Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo akiwa Mgeni Rasmi wa Mkutano wa Hadhara wa Kufunga Kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Kiti cha Uwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, huko Viwanja vya Mpira Daya, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
"Tumeendekeza ufisadi katika Nchi; sisi dhamira yetu ni kuimarisha utawala bora ambapo misingi yake ni njia pamoja na alama za utekelezaji wa haki, na kwamba kinyume chake ni sawa na kuukumbatia ufisadi, unafiki, uongo na ubadhirifu", amesema Mheshimiwa Othman.
Amekosoa na kutilia shaka mwenendo wa Chaguzi ndogo zilizopita hapa Visiwani, zikiwemo za Konde, Pandani na Amani, kwamba viashiria vyake ni dhidi ya misingi ya haki, na pia dalili za maandalizi ya vurugu, sasa na baadae katika Nchi.
Ametolea Mifano pingamizi zisizokuwa na Msingi dhidi ya Wagombea wa Upinzani, kuelekea Chaguzi hizo, kuwa niuthibitisho wa kukumbatia ufisadi, uongo, unafiki na ubadhirifu, mbele ya umma mkubwa wa wananchi.
Aidha, Mheshimiwa Othman amelitaja Jimbo la Mtambwe, akisema kuwa Uchaguzi wake siyo tu wa kumpatia kura Mgombea fulani, bali pahala pa kuitafuta Sauti ya Wananchi wote, wafuasi wa Vyama vyote vya Siasa, bila ya kujali itikadi zao, kutokana na Historia yake ya asili.
Akiweka msisitizo juu ya kuchunga misingi ya haki na uadilifu, na kuwacha ufisadi na ubadhirifu, Mheshimiwa Othman amesema, "hata hayo maendeleo hayawezi kuwa na thamani pindipo ikikosekana misingi ya haki ambayo hapana shaka ni njia ya kuelekea katika utawala mwema".
Akimuombea kura Mgombea wa ACT-Wazalendo katika Uchaguzi huo, Mheshimiwa Othman amewataka Wananchi wa Mtambwe wamchague, ili achukue dhamana ya kupaza sauti ya Wananchi wote, katika pahala ambapo ni Chimbuko la Muasisi wa Harakati Siasa za Upinzani Nchini, na Mtetezi wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
Hata hivyo, Mheshimiwa Othman amemtaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Hussein Ali Mwinyi, akisema, "iwapo ni muumini wa amani ya Nchi, awe mstari wa mbele katika kukemea ubadhirifu, ufisadi, uongo na unafiki, na pia kutetea misingi ya haki bila ya kujali maslahi ya kisiasa".
Mapema, Mheshimiwa Othman ameanza Ziara yake Jimboni hapo, kwa kumjulia-hali Mzee Masoud Marhun Aziz na mwanawe, Bw. Mohamed Masoud Marhun, kutokana na udhaifu wa afya zao, huko Nyumbani kwao, Kifumbikai, Wete Pemba.
Kabla ya hapo, Mheshimiwa Othman amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi mbalimbali wa Chama hicho, katika Ofisi za Jimbo la Mtambwe ziliopo Bwagamoyo, ambapo baada yake aliweza kutembelea na kubadilishana mawazo na Wanachama na Wafuasi wa ACT-Wazalendo, katika Barza ya Wazee na Vijana iliyopo Daya, pia Jimboni hapo.
Mheshimiwa Othman ambaye ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, yupo kisiwani Pemba kwa Ziara maalum ya Siku 4, kwaajili ya Shughuli mbalimbali za Chama na Serikali.
Naye, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Mhe. Salim Bimani ametoa angalizo akisema Tume Mpya ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) chini ya Mwenyekiti wake Jaji Joseph Kazi, kuwa Jimbo la Mtambwe kwa sasa litakuwa ni Mtihani wao wa Kwanza.
Katika Salamu zake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Bw. Ismail Jussa Ladhu akikariri uweledi ulioelezwa na Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume wa Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba, amesema Wananchi wa Zanzibar hasa kutoka kisiwani Pemba, hawana ulazima wa kufundishwa Siasa, kutokana Misimamo yao ya kutodanganyika na pia juu ya Uchungu wa Nchi.
Kwa upande wake, Mgombea wa ACT-Wazalendo, Bw. Mohamed Ali Suleiman, amewaomba wananchi wamkopeshe kwa kumchagua yeye, kwa kumpigia kura za NDIYO katika Uchaguzi huo, ili akatetee huduma za msingi zikiwemo, za maji na umeme, katika Jimbo hilo, sambamba na kusaidia kupaza sauti ndani ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, dhidi ya vitendo vyote vya ufisadi Nchini.
Viongozi mbalimbali wa Chama hicho wamehudhuria katika Mkutano huo wakiwemo Mratib wa ACT-Wazalendo kisiwani Pemba, Bw. Said Ali Mbarouk; Katibu wa Oganaizesheni na Wanachama, Bw. Omar Ali Shehe; Katibu wa Chaguzi, Bw. Muhene Said Rashid; Mshauri wa Chama, Bw. Juma Said Sanani; akiwepo pia Mjane wa Maalim seif Sharif Hamad, Mama Awena Sinani Masoud.
Mkutano huo umeambatana na harakati mbalimbali zikiwemo za Taaluma juu ya Upigaji-Kura, Dua ya Ufunguzi iliyosomwa na Sheikh Mohamed Khatib, zikitanguliwa na Utenzi na Burudani kutoka kwa Wasanii wa hapa kisiwani Pemba, akiwemo Bw. Vuale 'Wanlalahoa'.
Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mnamo Tarehe 28 Oktoba 2023, unakuja kufuatia Kifo cha aliyekuwa Muwakilishi wa Jimbo hilo Marehemu Habib Mohamed, kilichotokea mapema Mwaka huu.
Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Oktoba 26, 2023.
Post A Comment: