Na John Walter-Manyara
Afisa udhibiti ubora kutoka shirika la viwango Tanzania TBS Pius Mwakalinga, ametoa wito kwa wafanyabiashara hapa nchini kuhakikisha bidhaa zao zinathibitishwa na shirika la viwango kwani itasaidia bidhaa kuuzika kwa urahisi hapa nchini na nje ya nchi na kuwasaidia kukua zaidi kibiashara kwani wateja watapata uhakika wa ubora na usalama wa bidhaa wanazonunua.
Akizungumza katika maonesho ya biashara yaliyoandaliwa na chemba ya biashara , viwanda na kilimo Tanzania TCCIA kwenye uwanja wa stendi ya zamani mjini Babati mkoani Manyara Mwakalinga amesema ili kukuza biashara ni muhimu watanzania kupeleka bidhaa zao kwenye ofisi za shirika hilo ngazi ya kanda kwa lengo la kuhakikiwa na huduma ya kuhakiki bidhaa ni bure kabisa kwa kipindi cha miaka mitatu ya awali.
Aidha Mwakalinga amewashauri wafanyabiashara na wajasiriamali wanaotaka huduma ya kuhakikiwa viwango vya ubora wa bidhaa zao wapitie kwenye shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO kwani watapewa mafunzo mbalimbali na watapewa barua itakayowawezesha kutambuliwa mahali wanapotoka na biashara wanazofanya ili maafisa kutoka shirika la viwango waweze kuwatembelea kwa urahisi kwenye maeneo yao ya biashara na kuwapatia huduma.
“Serikali kupitia shirika la viwango Tanzania tunatoa huduma kwa wajasiriamali kwa miaka mitatu lakini pia tunawashauri wapitie SIDO, kule wanapewa mafunzo mbalimbali hivyo anavyokuja kwenye shirika la viwango Tanzania na barua ya SIDO itamwezesha kumtambulisha huyo mjasiriamali”
Kuanzia mwaka wa nne Mwakalinga amesema mfanyabiashara ataanza kulipia robo ya gharama za bidhaa alizonazo na kuhakikisha mfanyabiashara anakua kibiashara kabla ya kuanza kumtoza gharama za upimaji na kuthibitisha bidhaa.
Kuhusu udhibiti wa ubora wa bidhaa Mwakalinga amesema wanaendelea kufanya ukaguzi wa bidhaa ambazo tayari zimepimwa na kuthibitishwa ili kubaini kama bado zinaviwango au zimepunguzwa ubora kwani baadhi ya wafanyabishara hufanya uchakachuaji wa bidhaa hivyo amewaonya kuacha tabia hiyo maramoja kwani ukibainika utakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na sheria itafuata mkondo wake.
Udhibiti huo unakwenda sambamba kabisa na sheria ya viwango namba mbili ya mwaka 2009 inayoweka masharti ya uimarishaji wa viwango vya vipimo vya bidhaa na huduma, kuanzisha upya shirika la viwango Tanzania na kutoa masharti bora ya kazi, usimamizi na udhibiti wa ofisi, kufuata sheria ya viwango sura namba 130 na kutoa masharti mengine yanayohusiana.
Shirika la viwango la taifa ni shirika lililoanzishwa na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha miundombinu tegemezi kwa sekta za viwanda na biashara.
Nafasi ya shirika hilo ni kukuza viwango, usalama na uhakikisho wa ubora katika tasnia na biashara na kupitia ukuzaji wa viwango, uthibitishaji, usajili, ukaguzi, upimaji na huduma za vipimo kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Post A Comment: