MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inaandaa mkakati mpya wa ukusanyaji mapato utakaolenga kuongeza mapato ya Taasisi hiyo mara dufu ya makisio yake ya Mwaka wa fedha 2023/2024.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda katika kikao kazi na wakuu wa Kanda na wakuu wa mapori wa TAWA chenye lengo la kuboresha utendaji kazi katika nyanja za kuongeza mapato na Uhifadhi kwa ujumla, kilichofanyika  ukumbi wa Ngorongoro Crater Hall, Jijini Arusha.

Kamishna Mabula amesema suala la kuongeza Kasi ya ukusanyaji mapato ni maelekezo mahsusi kutoka kwa Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki na hivyo utekelezaji wake unapaswa kuanza haraka iwezekanavyo

"Hili suala la ukusanyaji mapato lisisubiri huo mkakati unaoandaliwa lianze Kuanzia Sasa hivi, Kila kitu unachokiona kwenye eneo lako ni rasilimali hakikisha unakitumia kuingiza mapato" amesisitiza Kamishna Mabula

Kamishna Mabula pia ametoa msisitizo katika suala zima la udhibiti wa Wanyamapori wakali na waharibifu na kuwataka maofisa hao kutafuta mbinu mbadala za kuhakikisha Wanyamapori hao hawaendelei kuleta madhara kwa maisha na mali za binadamu.

Aidha, amewataka maofisa hao kuzingatia maelekezo aliyoyatoa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili Kamishna Benedict Wakulyamba wakati wa semina elekezi kuhusiana na Wanyama Wakali na Waharibifu

Kwa Upande wake Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mlage Kabange amesema mtaji namba moja wa TAWA ni  ulinzi wa maeneo yote waliyopewa kuyasimamia kwani maeneo yanapokuwa salama ndipo uzalishaji mapato unaongezeka ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya mapato ya TAWA yanatokana na shughuli za Uwindaji wa Kitalii

Sanjari na hilo, amesisitiza kuongeza Kasi ya utekelezaji wa zoezi la kuweka alama za mipaka katika maeneo yote yaliyo chini ya Usimamizi wa Taasisi  huku wakifuata miongozo na maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali.














Share To:

Post A Comment: