Imeelezwa kuwa, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ni kitovu cha mafunzo katika tasnia za Sanaa na Utamaduni nchini na Serikali imeendelea kuiboresha taasisi hiyo kwa kutoa fedha za kuboresha miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Tamasha la 42 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lililoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na TaSUBa mkoani Pwani Oktoba 28, 2023.
"Niwapongeze Wizara kwa kuitangaza nchi yetu kwa kupitia kazi mbalimbali za utamaduni, sanaa na michezo. Aidha nakupongeza Waziri na wafanyakazi wa Wizara yako kwa kazi kubwa mnayoifanya kila mwaka katika kuliandaa na kuliendesha Tamasha hili kwa kipindi cha miaka 42 sasa," amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa, tamasha hilo lina hadhi kitaifa na kimataifa kwani limehusisha ushiriki wa vikundi vingi vya sanaa vya hapa nchini na vya kutoka nje ya nchi zikiwemo Zambia, Kenya, Burundi, Uganda, Botswana, Afrika Kusini, Canada na nyinginezo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameipongeza taasisi hiyo kwa kukuza utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) hapa nchini jambo linalofanya kuendelea kuvutia utalii wa ndani na nje ya nchi.
"Nawakaribisha na kuwahimiza vijana wote wa kitanzania wenye vipaji vya sanaa kuchangamkia fursa hii kwani sanaa sasa ni ajira hivyo tuitumie vyema kupitia taasisi hii," amesisitiza Dkt. Biteko.
Vile vile, Dkt. Biteko ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa na Mipango mikakati ya kuwasaidia wasanii nchini ili kupitia sanaa hiyo waweze kunufaika kiuchumi na kuitangaza nchi. Amesisitiza wapewe ushirikiano ili Sekta hiyo iwe na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa, tamasha hilo limekua na mafanikio makubwa kwa Bagamoyo na mkoa wa Pwani. Amesema wadau wamejitokeza kwa wingi na kulifanya liwe tamasha bora nchini.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kuwa, tamasha hilo ni fursa ya kutangaza utalii uliopo nchini kwa kuwakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi. Amesisitiza kuwa mwaka 2024 tamasha litakuwa kubwa kwa kuwaleta wadau wengi zaidi nchini.
Wengine walioshiriki kilele cha tamasha hilo ni Mkuu wa Chuo TaSUBa, Dkt.Herbert Makoye, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash na Watendaji wa Taasisi za Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wadau wa Sanaa na Utamaduni. Maonyesho hayo ambayo hufanyika kila mwaka yalianza rasmi tarehe 26 mwezi huu na kilele chake ilikuwa Oktoba 28, 2023.
Post A Comment: