Na: James Mwanamyoto, (OR-TAMISEMI)
OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafanya tathmini ya namna bora ya kukabiliana na majanga ya moto katika maeneo yao ili wawe na utayari wa kuyakabili pindi yanapojitokeza.
Maelekezo hayo yametolewa Oktoba 3, 2023 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwenye ziara ya kukagua eneo la wafanyabiashara la Kariakoo ambalo liliungua na moto siku ya Oktoba mosi, 2023.
Mhe. Ndejembi amewataka viongozi hao kuwa na utamaduni wa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira katika kuchukua hatua za dharura endapo likitokea janga la moto na kusisitiza kuwa, kwa upande wa Dar es Salaam uongozi wa mkoa na wilaya unapaswa kushirikiana DAWASA kufanya tathmini ya kuepukana na majanga ya moto.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewaomba wafanyabiashara walioathirika na janga la moto kuwa wavumilivu hadi kamati ya uchunguzi iliyoundwa itakapotoa taarifa za chanzo cha janga la moto lililojitokeza.
“Wafanyabiashara kuweni wavumilivu mpaka kamati ya siku saba iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa itakapotoa taarifa rasmi ya janga hilo ili kuiwezesha Serikali sikivu ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua stahiki na kuongeza kuwa, zimebaki siku nne tu kamati hiyo ikamilishe taarifa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Sanjari na hilo, Mhe. Ndejembi amewasilisha salamu za pole za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mchengerwa kwa wahanga wa janga hilo la moto ambao wamepoteza mali zao na kupata hasara kibiashara.
Post A Comment: