Na.Wizara ya Madini - DSM


Serikali ya Tanzania imesema  itaendelea kuipa umuhimu Sekta ya Madini ikiwemo kushirikiana na  Wadau wa Madini  katika kuendeleza mipango ya Taifa na kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo kwenye Sekta ya Madini nchini.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 26,2023 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa  alipomwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar katika kufunga Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji wa mwaka 2023.

Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali ipo tayari na inaruhusu miradi ya maendeleo kutoka Sekta binafsi katika Utafutaji , Uchimbaji , uchorongaji na uongezaji thamani madini ili kufanikisha mikakati iliyopo kwa  wachimbaji kwa wachimbaji wote nchini.

Mhe. Majaliwa amefafanua kuwa Serikali ina Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambazo zinafanya kazi ya utafiti , uchenjuaji na uchorongaji kwa kushirikiana na kampuni binafsi  na kutoa wito kwa wadau wote walioshiriki katika mkutano huo kutumia hizo za ushirikiano wa  kimkakati.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali kupitia Taasisi ya GST ina mpango wa kufanya utafiti wa jiolojia kwa nchi nzima ifikapo mwaka 2030  ili kuwa na kanziData ya  taarifa za jiolojia zitakazo tumika kuvutia  wawekezaji wa madini ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake , Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde amesema Wizara imetumia  Mkutano huo katika kukuza ushirikiano wa kikazi baina ya nchi na nchi kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa  kama vile majadiliano kuhusu matumizi ya Nishati safi ili kupambana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Mavunde ameongeza kwamba,  sekta ya madini inaendelea kusimamia miradi mbalimbali nchini ambapo leo Oktoba 26 , 2023 kampuni ya Noble Helium imeanza kutafiti na kuchoronga   Gesi ya Helium mkoani Rukwa.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema kwa katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara ya  Madini ilikusanya Shilingi Bilioni 678.

Awali , Mwenyekiti wa  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mathayo David Mathayo amesema kuwa kazi kubwa ya kamati ni kuishauri na kusimamia sekta ya madini ili ikamilishe malengo iliyojiwekea hivyo itaendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa Sekta ya Madini.

Mkutano wa Madini na Uwekezaji Tanzania kwa mwaka 2023 umeongozwa  na Kauli mbiu inayosema  Uncloking Tanzania's Future Mining Potential.


Share To:

Post A Comment: