.


 Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu Msingi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ,Josephat Luoga amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imekuwa ikitekeleza program na Mipango mbalimbali ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi kwa lengo la kuwa na Watanzania walioelimika.


Luoga ametoa kauli hiy wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima linalofanyika Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Amesema miongoni mwa program hizo ni pamoja na Mpango wa Elimu Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA), Mpango wa Elimu Sekondari kwa Njia Mbadala (AEP), Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (IPOSA).

Program nyingine ni Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu na Jamii (MUKEJA), Uzalishaji Mali (UMALI), Shughuli za Ugani (SU) pamoja na Village Community Bank (VIKOBA).

Akizungumzia historia ya Maadhimisho hayo, Luoga amebainisha kuwa tangu mwaka 1961, Tanzania imekuwa ikifanya juhudi mahususi katika kukabiliana na tatizo la kutojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

“Katika mwaka 1970 Mwalimu Julius Nyerere alitumia Elimu ya Watu Wazima kuzindua kampeni mbalimbali, ikiwemo Kisomo Chenye Manufaa (KCM), pamoja na program saidizi za kisomo kama vile Elimu Kwa Wafanyakazi” Alifafanua Luoga.

Nae Mratibu wa Kongamano hilo Dkt. Sempeo Siafu amesema Maadhimisho hayo yaliasisiwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mwaka 1966 ili kuikumbusha Jamii umuhimu wa Elimu ya Watu Wazima.

“Nawaasa wadau kutumia Kongamano hili kuangalia namna ya kuboresha Mazingira ya Ujifunzaji katika program za Kisomo yanayozingatia Ubora, Usawa na Ujumuishwaji wa Makundi yote” Alisema Dkt. Siafu.


Afisa Elimu mkoa wa Pwani, Sara Mlaki amesema mkoa huo unatekeleza programu mbalimbali kwa halmashauri zote kama vile Mpango wa Elimu ya Msingi kwa waliokosa MEMKWA jumla ya wanafunzi 1943 wakiwemo wavulana 1117 na wasichana 826 wamenufaika.


Ameongeza kuwa mkoa huo, unatekeleza program ya Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya watu wazima na Jamii MUKAJE yenye jumla ya wanafunzi 2080 ikitajwa kuwa program nzuri ya elimu nje ya mfumo rasmi kwani wanajifunza na shughuli za uzalishaji mali kama vile mapishi, ushonaji, mapambo, ufumaji, ususi na usindikaji.

Baadhi ya wanufaika wa programu ya Elimu ya watu wazima akiwemo Siri Kibinde amesema kwa sasa amejua kusoma na kufanya shughuli za ujasiriamali kama vile ushonaji,mapambo, ususi na usindikaji

Share To:

Post A Comment: