Na Elizabeth Joseph,Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh, John Mongella amewataka Waandishi wa Habari nchini kutumia vizuri mafunzo yanayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuhabarisha jamii habari zenye takwimu sahihi hasa Matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Kauli hiyo ameitoa Oktoba 24 jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya Wanachama wa Vyama vya Waandishi wa Habari kwa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania yaliyohusu Usambazaji na matumizi ya Matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Amesema kuwa sekta ya habari imekuwa na mchango mkubwa katika kufikisha ujumbe kwa wananchi wengi na kwa haraka ikiwemo taarifa za zoezi zima la Sensa hiyo hivyo ni muhimu kwa wanahabari hao kutenga muda stahiki katika kujifunza juu ya namna bora ya kusambaza Matokeo ya Sensa ili kufikisha taarifa zilizo na usahihi kwa jamii.
"Kupitia mafunzo haya mnayopewa na NBS itawasaidia Waandishi kutoa taarifa nzuri za Takwimu na hatimae kuondoa upotoshaji wa zoezi la Sensa kwa jamii ambao unachangiwa na kutokuwa na taarifa sahihi ambazo nyingine zinasababisha migogoro isiyo na lazima"ameongeza kusema Mkuu huyo wa Mkoa.
Naye Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Mh,Anne Makinda aliwataka wana habari hao kuhakikisha wanatenga muda wa kutosha katika kusoma na kuelewa taarifa za Takwimu jambo alilosema litaongeza uzito na kuaminika katika taarifa zao wanazohabarisha jamii.
"Takwimu ni hali halisi katika nchi yetu ili kupiga hatua katika mambo mbalimbali kimaendeleo,ninyi ni kundi muhimu lazima tushirikishe Waandishi wa Habari kuwafundisha matokeo ya Sensa na namna ya kuandika ili muwaeleweshe wananchi juu ya takwimu ili tuweze kufikia lengo na kuipeleka nchi yetu mbele"alisema Kamisaa huyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Sensa Mkoa wa Arusha,Bi Leokadia Mtei aliwaomba wanahabari hao kujenga mahusiano zaidi na Ofisi ya Takwimu kwakuwa kupitia ushirikiano huo kutawawezesha kupata taarifa sahihi na kwa wakati juu ya masuala ya Takwimu katika majukumu yao ya kazi.
Katika mafunzo hayo ya Siku mbili kuhusu Uwasilishaji, Usambazaji na Uhamasishaji wa matumizi ya Matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo vyanzo vya Takwimu,Matokeo ya Sensa kwa ujumla,matumizi ya Takwimu za kijiografia ya Sensa ya watu na makazi pamoja na matumizi ya Takwimu katika Habari.
Post A Comment: