Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa vituo vya Polisi cha Wilaya ya Ikungi na Mkalama katika hafla iliyofanyika Oktoba 15, 2023.Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Kamillius Wambura, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.

.........................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Ikungi na cha Wilaya ya Mkalama mkoani Singida na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kuacha mara vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.

Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa aliyoianza Oktoba 15, 2023 alipokuwa akifungua kituo hicho cha polisi alisema ujenzi wake umefanyika kwa thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali.

" Nimeambiwa humo ndani mna mambo mazuri mheshiwa IGP sina maswali kwenye thamani halisi ya gharama za ujenzi wa kituo hiki kwa kweli sina maswali nakupongeza, nawapongeza wabunge na jeshi la polisi kwa kazi nzuri na kupata jengo hili," alisema Rais Samia.

Rais Samia aliwaambia wananchi hapo ni makao makuu ya Polisi Wilaya ya Ikungi na ndani ya kituo hicho imejengwa miundombinu mizuri sana kwa ajili yao.

"Kwa wale wahalifu hapa patakuwa ni nyumbani kwao lakini yale mambo ya kuchukua sheria mkononi kwa sababu sasa jeshi la polisi lipo hapa sasa yaishe Serikali imejenga jengo zuri huduma itatolewa humo kwa hiyo wananchi hakuna sheria mkononi mambo yote yaletwe hapa yatashughulikiwa nisisikie tena watu wamechomana mishale," aliongeza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia aliwageukia watumishi wa jeshi la polisi na kuwaambia kuwa na jengo zuri ni jambo moja na la pili ni kuwa na huduma bora kwa wananchi.

" Unajua ukipata jengo zuri nimeambiwa mnanyumba za watumishi na wakubwa huko nyuma ni mahali pazuri na mnakaa vizuri na kupata moyo wa kufanya kazi nawaombeni muwatumikie wananchi kwa kuwapatia huduma nzuri," alisema Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkadiriaji Majengo wa Jeshi la Polisi Mkaguzi wa Polisi, Asha Tuwa ujenzi wa jengo hilo umezingatia miundombinu ya makundi mbalimbali ya watu wakiwamo wenye ulemavu na kuwa ujenzi wa vituo hivyo umegharimu Sh. Bilioni 2.

Rais Dkt. Samia baada ya kufungua kituo hicho alipata fursa ya kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi eneo la Puma na kuwaomba kesho Oktoba 16, 2023 wafike Viwanja vya Bombadia ambapo kutakuwa na mkutano mkubwa wa hadhara na kuzungumzia mambo mbalimbali.

Akitoa salamu kwa Rais Samia kwa niaba ya wanananchi Mbunge wa jimbo hilo, Elibariki Kingu alimshuru Rais kwa kazi kubwa aliowafanyika ya kuwapelekea miradi mingi ya maendeleo na ombi lake kubwa aliomba apewe Halmashauri ili iwe rahisi kuwatumikia wananchi kutokana na ukubwa wa jimbo hilo.



Viongozi hao wakiwa katika picha ya pamoja na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Wananchi wakiwa wamejipanga barabarani kumlaki Rais Samia wakati alipokuwa amewasili Shule ya Msingi Imbele kuizindua.

Msafara wa Rais ukiondoa baada ya uzinduzi wa shule hiyo.







Muonekano wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi kilichozinduliwa na Rais Samia.





Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kikitoa heshima kwa Amiri Jeshi Mkuu Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa gwaride la heshima walilomuandalia.

Wimbo wa taifa ukiimbwa.

Uzinduzi wa kituo cha Polisi Ikungi ukiendelea. Rais Samia akiwa na IGP Kamillius Wambura na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Wananchi wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Polisi cha Ikungi.
Share To:

Post A Comment: