Na John Walter-Manyara


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuchukua tahadhari na kujilinda na maambukizi ya UKIMWI kwakuwa bado ugonjwa huo upo na unaua.

Rais Samia ameyasema hayo aliposhiriki kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika mji wa Babati Mkoani Manyara ambapo pamoja na mambo mengine amewataka watanzania kujilinda na ugonjwa wa virusi vya Ukimwi kwani takwimu zinaonesha kwa mwaka watu elfu 29 hufariki kutokana na ugonjwa huo.

“Nawaasa Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya UKIMWI, pamoja na kwamba gonjwa hili sio janga tena , kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020/2021 wastani wa Watanzania elfu 54 wanapata maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI kwa mwaka na idadi ya vifo vinavyotokana na UKIMWI kwa mwaka ni takribani Watu elfu 29 sasa hii sio idadi ndogo, sio kama tulikotoka lakini hapa tulipofika hapajiridhisha niombe kila mmona ajilinde na janga hili” amesema Rais Samia.

UKIMWI bado unaendelea kuwa janga katika jamii yote ya dunia ikiwa imeshasababisha vifo vya watu takribani millioni 33 mpaka sasa kulingana na taarifa ya WHO ya mwaka 2020.

Mpaka mwaka 2019 takribani watu million 38 walikuwa  wanaishi na maambukizi ya VVU, Tanzania pekee ni watu millioni 1.6 wanaoishi na maambukizi hayo kwa taarifa ya mwaka 2018 pekee, hivyo taaarifa hizi zinaonyesha umuhimu wa kujikinga na maambukizi ya VVU. 

Wataalamu wa afya wanashauri Ili kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI ni muhimu kuondoa kabisa au kupunguza tabia hatarishi kwako ikiwemo kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja.

Matumizi ya kondomu za kike na kiume kwa uangalifu, ni vyema kutumia kondomu pindi unapojamiana na mtu usiye jua hali yake au mwenye maambukizi ya VVU. 

Tafiti zinaonyesha kondomu huzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo ukimwi kwa Zaidi ya asilimia 85. Zingatia uvaaji sahihi wa kondomu.

Aidha Tohara kwa wanaume imeonyesha kusaidia kupunguza maambukizi ya VVU kwa asilimia 60 na sio kuzuia kama ilivyodhana potofu ya watu wengi. 

Hivyo hakikisha kwa hiari unafanyiwa tohara mapema ili kupunguza hatari ya kupata maambubikizi.

Share To:

Post A Comment: