MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amekagua ujenzi wa shule ya sekondari mpya ya Kijiji cha Nkuhi kilichopo Kata ya Issuna na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake.


Shule hiyo ilipatiwa Shilingi Milioni 544 kutoka serikali kuu na nguvu za wananchi Shilingi Milioni 117 ili kujenga madarasa nane ,jengo la utawala,maabara tatu,chumba cha kompyuta,maktaba na matundu ya vyoo kwa ajili ya walimu na wanafunzi.


Akizungumza Octoba 3,2023 baada ya ukaguzi huo,Mtaturu amewapongeza kamati ya ujenzi kwa usimamizi mzuri kwa kushirikiana na viongozi wa Kata na Vijiji.


“Ndugu zangu niwapongeze sana kwa ushirikiano mliouonyesha katika kusimamia ujenzi huu, nimepita na kukagua nimeona kazi inaenda vizuri,hivi ndio inavyotakiwa,serikali inaleta fedha sisi viongozi na jamii tuwe na uchungu wa kusimamia ili mradi husika ukamilike kwa wakati na kwa thamani ya pesa iliyotolewa,kwak ufanya hivi tutakuwa tunaunga mkono juhudi za Rais wetu mpendwa Mh Samia Suluhu Hassan,”.amesema.


Akisoma taarifa Mwalimu Mkuu Msaidizi Obeid Simba kwa kwa niaba ya Mkuu wa shule ya Issuna amesema kukamilika kwa shule hiyo kutaondoa changamoto ya muda mrefu ya wanafunzi kutembea mwendo mrefu lakini pia itaepusha wanafunzi kuacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba zisizotarajiwa.


“Kwa niaba ya wananchi wa Vijiji vya Nkuhi na Tumaini tufikishie salaam za shukrani kwa Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu muhimu kwenye kijiji chetu,shule hii ikikamilika itaondoa changamoto iliyokuwepo ya wanafunzi kutembea umbali mrefu,”ameshukuru.


Akitoa shukrani Diwani wa Kata ya Issuna Stephano Misai amempongeza Mbunge Mtaturu kwa kupaza sauti na hatimaye kero ya watoto kutembea zaidi ya Kilomita 9 kufuata shule Issuna inaenda kuisha.


“Mbunge wetu unafanya kazi kubwa sana,umekuwa mdomo wetu wa kutusemea kero na shida zetu na hatimaye kupatiwa ufumbuzi,tumeona juhudi zako kwenye sekta mbalimbali serikali imeleta fedha na wananchi wanapata maendeleo,ila kwenye hili nakupongeza zaidi maana watoto wetu wanaenda kuondokana na adha ya kutembea mwendo mrefu,”.amesema.


Ujenzi huo ulikuwa ukamilike Septemba 30 mwaka huu lakini kuna changamoto ya upatikanaji wa maji karibu na umeme imechangia kuchelewa kukamilika kwa wakati.    
Share To:

Post A Comment: