Na John Walter-ManyaraWaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amewaagiza wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wa mikoa kote nchini kuhakikisha wanawasaidia vijana kufika mkoani Manyara kwa ajili ya Kongamano la wiki ya vijana kitaifa linalotarajiwa kufanyika mkoani humo kuanzia tarehe 8 Oktoba Hadi tarehe 14 Oktoba 2023.
Ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua maandalizi ya eneo litakalofanyika Kongamano hilo katika uwanja wa stendi ya zamani mjini Babati.
Profesa Ndalichako amesema kuwa kupitia Kongamano hilo vijana watakaoshiriki watapata fursa Mbalimbali ikiwemo kupewa Elimu ya kujiajiri ili kupunguza changamoto ya Ajira nchini inayowakabili kwa sasa.
Aidha akiwa ameambatana na mkuu wa mkoa na kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapa, wamekagua uwanja wa Kwaraa yatakapofanyika maadhimisho hayo, Kanisa la Parokia Mtakatifu itakapo fanyika ibada ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na uwanja wa stendi ya zamani itakapo fanyika wiki ya vijana.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2023 zinaongozwa na kauli mbiu isemayo “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai na Uchumi wa Taifa”
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amewataka Vijana kuhudhuria kwa wingi katika wiki hiyo ya vijana ambayo itakuwa na mijadala mingi itakayowavusha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Post A Comment: