Na John Walter-Mbulu
Wananchi zaidi ya 7,640 wa kijiji cha Labay Kata ya Labay Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama baada ya Mwenge wa uhuru kuzindua Mradi mkubwa wa maji wa Kijiji hicho uliotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.069.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ni ya nne kati ya Halmashauri saba za mkoa wa Manyara ambako Mwenge wa uhuru unakagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya jumla ya shilingi Bilioni 1.8 na kuzinduliwa kwa mradi huu wa maji ni ishara ya ukombozi wa Wananchi wa kijiji hicho na Vitongoji vyake.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Mbulu Mhandisi Onesmo Mwakasege amesema kukamilika kwa mradi huo kumeongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia 89.
Akizungumzia mradi huo kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaib Kaim, amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwezesha RUWASA kukamilisha mradi huo, huku Wananchi wa Labay wakisema umewakomboa na utumiaji wa Maji ya visima ambayo nayo yalikuwa wanayafuata mbali.
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 inasema “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa”,
Post A Comment: