Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Mariam Ditopile amegawa mitungi 250 ya Taifa gesi ya kupikia kwa Jumuiya ya Wanawake Tanzania( UWT) Wilaya ya Kondoa, lengo likiwa kumtua mama kuni kichwani.
Aidha uamuzi huo wa kugawa mitungi hiyo ni kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuondoa nishati chafu ya kupikia kama kuni na mkaa na jamii itumie nishati safi kama gesi ya kupikia.
Mariam amegawa mitungi hiyo leo Oktoba 13, 2023 wilayani Kondoa, wakati akizungumza na wanawake wa UWT ambao wanaadhimisha wiki ya UWT katika Wilaya hiyo.
"Leo tuko hapa katika maadhimisho ya UWT Wilaya ya Kondoa na kila mwaka huwa tufanya wiki ya UWT kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa mpaka Taifa.
"Tulikuwa Chemba wiki iliyopita na kisha tumeenda wilaya nyingine na leo tuko Kondoa na ni utamaduni wetu kufanya mambo kadha wa kadhaa ya kijamiii ikiwemo kutembelea wagonjwa, " amefafanua Ditopile.
Akifafanua zaidi katika kuadhimisha Wiki ya UWT ameona ni vema akafanya jambo ambalo limeasisiwa na Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan mwaka 2022 kupitia Wizara ya Nishati ambapo kulifanyika kongamano la kuhamasisha
nishati safi ya kupikia.
"Katika siku hiyo mbele ya Rais wetu mpendwa Dk.Samia tulijadili namna gani tunamtua kuni mama kichwani na bahati nzuri nami nilikuwepo kwani nilikuwa katika Kamati ta Nishati na Madini, tulioneshwa video tulielimishwa.
"Tunataka kumkomboa mwanamke lakini kuni zinaua sana mama zetu , kuni zinaleta matatizo makubwa kwa mama zetu, Serikali yetu kupitia Rais Samia ameendelea kutafuta nishati safi ya kupikia. Akiwa Makamu wa Rais alipambana na kumtua ndoo mama kichwani na leo tunaona matunda yake, " amesema.
Amewaeleza wanawake hao wa UWT kwamba mitungi hiyo ambayo ameigawa leo inatokana na fedha za Samia Suluhu Hassan ambaye ni jasiri muongozaa njia kwani kupitia Bunge alileta bajeti ya ruzuku ya kununua mitungi ya gesi na asigawe yeye ipite kwa wabunge.
"Sisi ni nani tusirudishe sifa kwake, nikasema kwanini nikagawe mitungi ya gesi uchochoroni, najua ni kidogo lakini kila mtu ajue Rais wake amemkumbuka, hivyo tumegawa kwa uwazi ili watu waione, watakaopata watashukuru na wasiopata tutatafuta mingine" amesema.
Aidha amesema ugawaji huo wa mitungi ni sehemu ya kuhamasisha kampeni ya nishati safi ya kupikia ambayo inafanyika nchi nzima huku akifafanua katika kuendeleza jitihada hizo tayari Rais Samia amewekeza, kwani kuna mradi wa kuzalisha gesi yetu wenyewe kutoka Mtwara , na tayari mikataba ya awali imeshasainiwa.
"Pale Ikulu Chamwino Dodoma tulienda kushuhudia utiwaji saini mkataba wa kuwekeza kiwanda cha kuchakata gesi ya LNG kule Lindi ile gesi itakapokamilika itakuja mpaka Kondoa, ni ndoto yake Rais na sisi tukimuunga mkono na kumuongeza ataitimiza. Tutakuwa na gesi majumbani kwetu."
Post A Comment: