Mbunge wa  Jimbo la Siha,  ambaye  pia  ni Naibu  Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga shule katika kila kijiji ili kuwapunguzia watoto adha ya kutembea mwendo mrefu kwenda shule.

Dkt. Mollel amebainisha hayo wakati akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo iliyoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika  Jimbo la Siha ambapo amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wanapeleka watoto shule ili kupata elimu.

Amesema Rais Samia katika jimbo la Siha ameupiga mwingi hususani kwenye kuboresha miundombinu ya elimu na madarasa mengi yamejengwa katika shule zilizokuwa zimechakaa na kuleta taswira mpya katika jimbo hilo.

“Mpaka sasa tumebaki na vijiji vichache sana ambavyo havijapata shule ila naimani kubwa kwa dhamira ya kiongozi wetu Dkt. Samia kabla ya 2025 atakuwa ameweka mambo safi”, ameeleza Dkt. Mollel

Aidha ameeleza kuwa serikali imara ya Dkt. Samia inaendelea kuhakikisha  inaleta maendeleo kwa wananchi wake kwa kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji pamoja na umeme ili kuwatia moyo wananchi kuendelea kufanya maendeleo katika taifa lao.

Katika sekta ya afya amesema kuwa upatikanaji wadawa umeongezeka ambapo kila watu 10 wanaopata dawa watatu ndio wanao kosa dawa tofauti na ilivyo kuwa awali.

Dkt. Mollel amesema kuwa kabla ya kufanya mkutano wa Jimbo amechukua jukumu la kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jimbo lake ili kuona maendeleo ya miradi hiyo imefikia wapi na kuhakikisha anatatua changamoto zote zilizopo katika kutekeleza miradi hiyo kukamilika.






Share To:

Post A Comment: