Angela Msimbira OR-TAMISEMI


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema serikali haitasita kuwachukulia hatua Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu na  Maafisa Elimu wa Halmashauri watakaoshindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa miundombinu ya elimu kwenye maeneo yao.

Akifungua kikao kazi cha Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri leo Oktoba 2, 2023 kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa,  amesema kuanzia sasa serikali haitamvumilia kiongozi yeyote ambaye hatatimiza majukumu yake kikamilifu hasa katika suala zima la usimamizi wa miradi.

Amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu nchini lakini wapo baadhi ya viongozi wamekuwa hawasimamii miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati.

“Fedha nyingi zinazotolewa na serikali kwaajili ya miradi ya elimu katika maeneo yenu kwani kila Halmashauri nchini imepewa fedha, na kama miradi haitekelezeki kwa wakati maana yake wewe hutoshi katika nafasi hiyo,”amesema.

Kadhalika, ameagiza uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza uanze mara moja Oktoba mosi hadi Desemba 31 mwaka huu ili shule zinapozinduliwa Januari mwakani wanafunzi waanze masomo mara moja.

Aidha, amewaagiza kuhakikisha waajiriwa wapya wanapata fedha zao kwa wakati kutokana na kuwapo na malalamiko kuwa kuna walimu bado hawajapata.

Share To:

Post A Comment: