Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dkt Charles Mwamaja (katikati) akiwasili katika hafla ya kutangaza matokeo ya hatifungani ya kijani ya Benki ya CRDB ‘Kijani Bond” iliyofanyika hoteli ya Johari Rotana ambapo Benki ya CRDB imetangaza kukusanya Shilingi bilioni 171.82 sawa na asilimia 429.57 ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 40 ambazo zitaelekezwa katika kufadhili biashara na miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Kamishna alipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia), na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (kulia).

========   =======  ========

Benki ya CRDB imetangaza matokeo ya mauzo ya hatifungani yake ya kijani ‘Kijani Bond’ iliyoweka historia ya kuwa hatifungani ya kwanza ya kijani nchini na kubwa zaidi kusini mwa Jangwa la Sahara katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.

Kijani Bond iliyozinduliwa Septemba 1, 2023 na kufungwa Oktoba 6, 2023, imekuwa na mwitikio mkubwa na hivyo kupelekea kufikia lengo kwa asilimia 429.57 ambapo jumla ya Shilingi 171.82 bilioni zimekusanywa ikilinganishwa na lengo la awali la TZS 40 bilioni. Kati ya wawekezaji 1,754 waliowekeza kwenye hatifungani hii, asilimia 99 ni Watanzania. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dkt Charles Mwamaja aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wa Fedha, Dkt Mwigulu Lameck Nchemba ameiopongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu na juhudi ilizochukua kuitoa na kuiuza hatifungani hiyo.
Dkt Mwamaja amesema idadi kubwa ya wawekezaji waliojitokeza kuwekeza kwenye hatifungani hii inadhihirisha juhudi kubwa zilizofanywa na Benki ya CRDB na fedha zilizopatikana zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea utekelezaji wa ajenda za maendeleo na juhudi za kulinda mazingira.

Kamishna Mwamaja pia amesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi sio tu unahitajika, bali haukwepeki kwani mahitaji ni makubwa.
"Tanzania inahitaji takriban dola bilioni 19.2 za Marekani mpaka mwaka 2030 ili kutoa mchango wake unaohitajika katika vita dhidi ya uharibifu wa mazingira. Sehemu kubwa ya fedha hizi inatakiwa itolewe na sekta binafsi. Kwa niaba ya Serikali, napenda nawapongeza kwa juhudi mnazozifanya ikiwamo Hatifungani hii ya Kijani na nyinginezo kama vile Programu ya Matumizi ya Teknolojia Endelevu za Kilimo Tanzania (TACADTP) mnayoshirikiana na Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNGCF),” amesema Dkt. Mwamaja.

Akiwashukuru wawekezaji waliojitokeza kwa imani waliyonayo na ushirikiano walioutoa hata kuwezesha mauzo hayo kuvuka malengo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kiasi kilichokusanywa kimeongeza mtaji mpya ndani ya taasisi hiyo kwa Shilingi bilioni 140 zitachochea utoaji wa mikopo kwenye miradi inayolenga kulinda mazingira nchini.

Mikopo hiyo sio tu itaongeza upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana na kukuza uchumi, Nsekela amesema zitadhihirisha utayari na umakini wa Tanzania kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye. 

“Ongezeko hili la mtaji wa Benki yetu ya CRDB litatuwezesha kutoa fedha zinazohitajika kwenye miradi tofauti inayojihusisha na kutunza mazingira kama vile viwanda endelevu, nishati safi, ujenzi na usafirishaji, maji, afya na elimu. Nawaomba wawekezaji wa ndani na kimataifa muendelee kushirikiana na benki yetu kufanikisha miradi hii,” amesema Nsekela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, ameipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio iliyoyapata na kusema hatifungani hii ya kijani imetolewa kwa muda muafaka kukidhi mahitaji yaliyopo.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, Kijani Bond iliorodheshwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili kuuzwa katika soko la upili. Akizungumza wakati wa uorodheshaji wa hatifungani hiyo sokoni, Kaimu Afisa Mtendaji wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Mary Mnisawa amesema mauzo ya hatifungani ya Benki ya CRDB sio tuimeinufaisha taasisi hiyo bali soko zima la fedha nchini.

“Kuorodheshwa kwa Kijani Bond kutakwenda kuongeza uuzaji na ununuaji wa dhamana katika soko hilo mara dufu kutoka wasatani wa sasa wa Shilingi bilioni 150 hadi zaidi ya Shilingi bilioni 300,” alisema Mniwasa.
Mkuu wa Idara ya Uchumi katika Ubalozi wa Uingereza nchini, Euan Davidson amesema Uingereza inayo furaha kubwa kufanikisha kutolewa hata kuuzwa kwa Hatifungani ya Kijani ya Benki ya CRDB. Mchango wa taifa hilo umetolewa kupitia taasisi ya FSD Africa iliyokuwa mshauri huru katika mchakato mzima wa kutoa mpaka kuuzwa kwa Hatifungani ya Kijani. Hayo yote yalifanyika yakiwezeshwa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (UK Development).

“Historia iliyoandikwa katika mauzo ya hatifungani hii kwa wingi wa wawekezaji binafsi hata mashirika yanadhihirisha kukubalika kwa sekta ya fedha ya Tanzania na kuonyesha kwamba kuna uhitaji mkubwa wa fedha za kufanikisha miradi ya mazingira mwongoni mwa wawekezaji tofauti, wa ndani na kimataifa,” amesema Davidson. 

Shirika la IFC lililo chini ya Benki ya Dunia ni miongoni mwa wawekezaji waliotoa kiasi kikubwa kwenye mauzo ya hatifungani hii. Shirika hilo pekee limewekeza Shilingi ambazo ni sawa na dola milioni 20 sawa na asilimia 29.3 ya uwekezaji wote uliofanyika.

Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki IFC, Jes Chonzi amesema: “Upatikanaji wa fedha za kufanikisha miradi inayolinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni fursa iliyo wazi kwa Tanzania na fedha nyingi zinahitajika hasa kutoka sekta binafsi. Hatinfungani hii itaongeza upatikanaji wa mikopo kwenye miradi ya mazingira na kuongeza ujumuishaji wa wananchikatika uchumi.”

Katika mchakato wa kutolewa na kuorodheshwa kwa Kijani Bond, Benki ya Stanbic Tanzania imeshiriki kama msimamizi mkuu, huku kampuni ya Denton Tanzania Law Chamber ikitoa huduma za ushauri wa kisheria. Kampuni ya Orbit Securities Tanzania ilikuwa wakala mfadhili, huku KPMG ikikabidhiwa majukumu ya kutoa taarifa za kihasibu.

Kijani Bond ni awamu ya kwanza ya mpango wa dhamana ya uwekezaji ya Benki ya CRDB wenye thamani ya dola za marekani milioni 300 unaolenga kukusanya fedha kwa ajili ya ufadhili miradi ya kijani, kijamii na endelevu. Benki ya CRDB imejitolea kuendeleza ukuaji wa uchumi wa kijani na shirikishi nchini kupitia ufadhili bunifu na rafiki kwa mazingira.















Share To:

Post A Comment: