Kardinali Protase Rugambwa

NA MWANDISHI WETU, ITALIA

WATANZANIA wameaswa kukaa pamoja na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kama njia ya kufanikisha maendeleo kwa Taifa.

Hayo yamesemwa na Kardinali Protase Rugambwa juzi wakati ameandaliwa hafla ya kupongezwa baada ya kusimikwa ukardinali na Kanisa Katoliki, ikiwa ni siku chache tu baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kumpongeza Mtanzania huyo wa tatu kutawazwa kofia hiyo ya Ukardinali, ambapo pia ni Askofu Mkuu Mwandamizi Jimbo Kuu la Tabora.


“Huu ni mwaliko wa kuendelea kujifunza kujenga umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, ili watu wote waweze kufurahia maisha na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani,”Alisema Kardinali Rugambwa.


Wakati anamtumia salamu za pongezi Kardinali Rugambwa, Rais Samia pia alijikita kwenye kauli mbiu ya kiongozi huyo kama njia sahihi ya kuelezea namna ya utumishi wa kiroho wa kiongozi huyo wa dini nchini Tanzania.


"Enendeni ulimwenguni kote", ikiakisi mafundisho ya Yesu Kristo katika Injili ya Marko 16:15, juu ya utume unaojali watu wote, sehemu zote na wakati wote. Naungana na Watanzania wote kukuombea kheri, afya njema, na mafanikio katika utumishi wako,” alisema Rais Samia, akiungana na Watanzania wengi waliomtumia salamu za pongezi Askofu Mkuu huyo wa Jimbo la Tabora.


Akizungumzia zaidi kuteuliwa kwake, Kardinali Rugambwa aliwashukuru waliotumia salamu za pongezi na upendo pamoja na kumtakia kheri katika maisha na utume wake tangu Baba Mtakatifu Francisco alipotangaza Makardinali wapya 21, huku yeye akiwa miongoni mwao.


Naye Balozi wa Tanzania, nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo, aliwasilisha salamu za pongezi za Rais Samia kwa Kardinali Rugambwa, huku akiwataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha wanaliombea mema Taifa pamoja na viongozi wake kama njia ya kudumisha amani, umoja, mshikamano na upendo kwa wananchi wote.

“Rais Samia anaungana na Watanzania wote kumwombea Kardinali Protase Rugambwa kheri, afya njema na mafanikio katika utumishi wake ambao unaongeza historia nzuri kimataifa kwa kuwa Mtanzania wa tatu kusimikwa Ukardinali,”Alisema na kuongeza.


“Wakati namtakia kheri na baraka tele Kardinali Rugambwa katika maisha yake ya utume kama Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, niwaombe pia viongozi wa dini wote waliombee Taifa letu ili kwa pamoja tushikiri kupiga hatua kubwa kimaendeleo,” alisema Balozi Kombo.

Julai 9 mwaka 2023 Baba Mtakatifu Francisko Dominika, alitangaza majina mapya ya Makardinali 21 huku watatu kati yao wakiwa ni wale waliojipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu kwa ujumla.

Share To:

Post A Comment: