Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) leo amekutana na Kamati ya kitaifa ya Maandalizi ya Onesho la Kimataifa la Swahili International Tourism Expo (Site!) na kukagua maandalizi ya Onesho hilo litakaloanza Oktoba 6 hadi 8 ,2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho ambapo aliambatana na Naibu wake Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, Mhe. Kairuki amewataka waoneshaji wote kuzingatia taaluma ili kuweza kuzielezea Taasisi zao kwa ufasaha.
"Mtu anayekuwa kwenye banda lazima awe mzoefu, anayeaminika na awe anajua anafanya nini, lengo ni kuijenga sekta hii ya Utalii" Mhe. Kairuki amesisitiza.
Aidha, amewataka waandaaji wa onesho hilo kuwa na utaratibu wa kujiendeleza kupitia fursa za mafunzo kwa njia ya mtandao.
"Tutumie vizuri mafunzo kwa njia ya mtandao yanayohusu masuala ya utalii katika kujiendeleza na kujifunza zaidi ili kuijua zaidi sekta hii" Mhe. Kairuki amesema.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amewataka waandaaji hao kuhakikisha wanaitangaza Tanzania kama nchi na sio taasisi mojamoja za Wizara ya Maliasili na Utalii.
Onesho hilo litahudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Afrika wakiwemo wanunuzi wa bidhaa za utalii ambao hutembelea maonesho ya Utalii kwa lengo la kujenga ushirikiano wa kibiashara na wafanyabiashara katika nchi husika.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa Wakurugenzi na baadhi ya watumishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania, TANAPA, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA)na wadau kutoka Sekta Binafsi.
Post A Comment: