Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais , Muungano na Mazingira, Dkt.Selemani Jafo amewataka vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani kuinua sauti na kuelezea wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la hasara na uharibifu unaohusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amewataka vijana kuwa mabalozi wa kampeni ya nishati safi ya kupikia na teknolojia, kuendeleza usawa wa kijinsia kwa wanawake wa vijijini na vijana katika nchi zinazoendelea, na kuchukua jukumu la kuhamasisha mabadiliko. Huku akitaka kuona mfuko wa Hasara na Uharibifu unafanya kazi haraka iwezekanavyo, na kupatikana kwa nchi zote zinazoendelea.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ameyasema hayo jana 4 Oktoba, 2023 alipofungua Kongamano la pili la Kimataifa la Viongozi Vijana na Mabadiliko ya tabianchi (GLOBAL YOUTH CLIMATE SUMMIT) lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Dkt. Jaffo amesema kongamano hilo ni jukwaa la kipekee ambapo vijana wenye ujuzi tofauti wanakutana kwa lengo la kuongeza uelewa wao wa sayansi ya mabadiliko ya tabianchi, kukuza uongozi, na kutengeneza suluhisho zitakalopeleka kuzuia na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Adha, Mheshimiwa Dkt. Jaffo amewataka washiriki wa kongamano hilo kubadilisha mtazamo wao kutoka kwenye utayarishaji wa nyaraka kuwa vitendo kwenye ngazi ya jamii. Huku akikipongeza Kituo cha Uongozi wa Vijana wa Kimataifa (Global Youth Leadership Center), kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu wa Tanzania (TFS) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa juhudi zao za kuwawezesha vijana na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za uchumi wa kijani na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Jaffo anasema vijana wa leo wana nafasi ya pekee katika utawala wa dunia huku akisisitiza umuhimu wa majadiliano yanayozingatia jinsi nchi zilizoendelea zinavyoweza kupata rasilimali muhimu ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha maendeleo endelevu kitaifa na kimataifa.
Anasisitiza umuhimu wa kugawana kwa haki bajeti ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu duniani kote, kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa katika mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Paris huku akiitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada kwa maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika mikakati ya kitaifa na mipango ya nchi zinazoendelea.
Anaongeza kawa anatarajia kwamba sauti za vijana hao zitaenea mbali, na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kupigana na mabadiliko ya tabianchi duniani.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu wa Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo amesema Kongamano hilo linalohudhuriwa na takriban washiriki 500 kati yao 200 wanashiriki moja kwa moja kutoka nchi 24 duniani na wengine 300 wanajiunga kwa njia ya mtandao linalenga kujenga uwezo wa vijana na kuwaandaa vijana viongozi katika mapambano ya mabadiliko ya tabianchi duniani.
“Tumechukua jukumu la kuwekeza kwa vijana kwa sababu vijana wanarithi matendo ambayo yalifanywa na warithi wetu na hivyo tunalizimika kuwaandaa sasa ili wayalinde mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu stahimilivu,” anasema Prof Silayo.
Naye Prof. Joel Nobert ambaye ni Mkurugeni wa Taasisi ya Rasilimali (Institute of Resource Assment) ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam anasema Kongamano hilo ni muhimu kwa vijana kwa kile alichoeleza kuwa linakwenda kuamua hatma ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi duniani.
Lucky Michael ni mshiriki wa kongamano hilo toka nchini anasema kupitia kongamano hilo watapaza sauti duniani kote kueleza athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuifanya dunia kuwa sehemu salama.
Post A Comment: