Na. Asila Twaha, OR- TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Majiji na Manispaa kutenga fedha zitakazowezesha watumishi kushiriki kikamilifu Michezo ya Watumishi wa Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA).
Dkt. Msonde ameyasema hayo leo Oktoba 30, 2023 wakati wa kufunga michezo ya SHIMISEMITA katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Amesema ni muhimu watumishi wote washiriki kwenye michezo ili wawe na afya njema yenye kuleta ukakamavu, weledi, umoja, upendo, ushirikiano, mshikamano na uzalendo.
"Michezo pia husaidia kuondoa msongo wa mawazo" amesema Dkt. Msonde
Amesema ni muhimu watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa washiriki katika michezo na kuimarisha michezo mahala pa kazi.
Pia Dkt. Msonde amewakumbusha watumishi hao kufuata taratibu za kiutumishi katika michezo hiyo na kuacha kuwaingiza watu ambao sio watumishi.
"Msiwashirikishe watu ambao sio watumishi michezo hii kwa ajili ya watumishi wa Serikali za Mitaa, kwani mkifanya kinyume chake mtakuwa mnavunja na kukiuka taratibu na maadili ya utumishi."
Aidha, Dkt. Msonde ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao kutumia michezo hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika mwaka 2024.
" Tumieni michezo kutoa hamasa na kuwakumbusha wananchi wote wenye sifa washiriki na kujitokeza katika uchaguzi."
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Michezo ya Watumishi wa Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) Bw. Jeshi Lupembe ameishukuru Ofisi ya Rais -TAMISEMI kwa kusimamia na kuwaruhusu watumishi hao kushiriki michezo.
Pia ameiomba Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuendelea kuzihimiza Halmashauri ziruhusu watumishi hao kushiriki pindi michezo hiyo inapofika sababu amesema, kwa mwaka 2023 kati ya Halmashauri 184 za Tanzania Bara ni Halmashauri 70 tu ndio zimeshiriki.
Post A Comment: